• Nairobi
  • Last Updated September 26th, 2023 10:25 PM
CECIL ODONGO: Ni unafiki serikali kutaka Raila awekewe vikwazo

CECIL ODONGO: Ni unafiki serikali kutaka Raila awekewe vikwazo

NA CECIL ODONGO

BAADA ya uchaguzi mkuu wa 2007, William Ruto pamoja na Uhuru Kenyatta walishiriki msururu wa mikutano ya maombi kuhusu mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kule Hague, Uholanzi, wakati huo.

Wakati wa mikutano hiyo, Ruto (sasa Rais) na Uhuru (Rais Mstaafu) walimlaumu kinara wa ODM, Raila Odinga, kwa madai ya kushirikiana na baadhi ya mataifa ya nje kufaulisha kesi dhidi yao.

Wawili hao wakati huo walikariri kuwa Kenya ni nchi huru yenye uwezo tosha wa kutatua masuala yake ya ndani bila kuingiliwa na nchi za ng’ambo.

Hata hivyo, mambo yamebadika na ni kinaya kwamba sasa utawala wa Rais Ruto anakimbilia mataifa yayo hayo akiyataka yamwekee Bw Odinga vikwazo vya kusafiri nchi za Magharibi.

Serikali inaona mbinu hiyo kama njia ya kumdhibiti Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye wanadai anatatiza uongozi wao.
Bw Odinga amekuwa akiendeleza mikutano ya maasi dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza, ambao unaonekana umeshindwa kutimiza ahadi tele ilizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni ikiwemo kupunguza gharama ya maisha kwa Wakenya.

Mwanzo, kwa kutaka Amerika na nchi za Magharibi zimwekee Raila vikwazo ni unafiki kutoka kwa serikali ambayo viongozi wake wamewahi kushutumu mataifa hayo kwa kuingilia masuala ya ndani ya Kenya.

Pili, ni kweli kwamba changamoto kama gharama ya maisha ya juu ni mambo yanayowakabili Wakenya.

Kama kiongozi wa upinzani, serikali haimtarajii Raila akimye tu huku Wakenya wakiendelea kuumia na kulemewa.

Kwa hivyo, ni uongo kudai kuwa mikutano hiyo ni ya kuyumbisha utendakazi wa serikali kwa sababu tangu uanzishwe, hakuna ghasia au uharibifu wa mali ambao umeripotiwa.

Jinsi hali ilivyo kwa sasa maisha ni magumu kwa kila Mkenya iwe alipigia kura serikali au la na hata waliounga serikali wameanza kuingiwa na wasiwasi kuhusu utendakazi wa utawala waliouchagua.

Tatu, suala la Raila kuachishwa kazi ya Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) halifai kutumika kurai nchi za Magharibi kumwekea vikwazo.

Iwapo mwishowe Odinga atawekewa vikwazo hivyo, hilo halitasaidia serikali kivyovyote kukomesha maasi dhidi yake iwapo gharama ya maisha itaendelea kumzidi raia wa kawaida.

Kuhusu kufunguliwa kwa mitambo ya IEBC, pia ni haki ya Odinga kusaka ukweli na amewahi kutoa sababu zake ambazo zimefanya asikubaliane na uamuzi huo wa Mahakama ya Juu kuhusu matokeo hayo.

Aidha, mataifa ya Magharibi hata Amerika yana sheria zao ambazo zinaamua iwapo kiongozi wa nchi fulani anawekewa vikwazo vya usafiri au hata mali yake katika nchi hizo kutwaliwa.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali itilie mkazo elimu ya wanafunzi wa Gredi...

WANDERI KAMAU: China Square: Tunahatarisha sifa ya Kenya...

T L