• Nairobi
  • Last Updated February 23rd, 2024 12:15 PM
CECIL ODONGO: Raila aingilie kati na kuzima uhasama kati ya Orengo na naibu wake

CECIL ODONGO: Raila aingilie kati na kuzima uhasama kati ya Orengo na naibu wake

NA CECIL ODONGO

KAUNTI ya Siaya ni miongoni mwa majimbo ambayo yanaheshimika nchini kutokana na kuwa chimbuko la viongozi mahiri ambao mchango wao aula kuhusu masuala mbalimbali umehisiwa pakubwa nchini.

Ukizungumzia mkondo wa mabadiliko ya kisiasa nchini basi kuna vigogo wasifika wa kisiasa kama marehemu Jaramogi Oginga Odinga, Achieng’ Oneko, Raila Odinga, James Orengo, marehemu Oki Ooko Ombaka, Odongo Omamo na wengineo.

Mchango wa wanasiasa hao katika kupigania uhuru wa Kenya na mfumo wa vyama vingi maarufu kama ukombozi wa pili u wazi. Aidha, kaunti hii inajivunia wasomi wengi, ambao ni mawakili, madaktari na maprofesa hasa katika eneobunge la Gem.

Hii ni kutokana na sera ya Chifu Odera Kang’o ambaye alishirikiana na wakoloni kufanikisha elimu ya kimisheni kwa Waafrika. Licha ya utajiri wa wasomi na viongozi wazalendo, ni jambo la kusikitisha kuwa jimbo hili limesalia nyuma kimaendeleo kutokana na mzozo wa mara kwa mara kati ya wanasiasa.

Wiki jana, vurugu zilishuhudiwa katika hafla moja ya mazishi ambapo wafuasi wa Gavana James Orengo na Naibu wake William Oduol Denge walirushiana makonde na viti kutokana na tofauti za kisiasa na usimamizi wa kaunti.

Mabw Orengo na Oduol wamekuwa na uhasama mkubwa kati yao ilhali ni miezi minane tu tangu Wakenya washiriki uchaguzi.

Uhasama huu bila shaka utapiga breki juhudi za utoaji huduma kwa raia kwa miaka mitano ijayo. Yamkini ndoa kati ya wanasiasa hawa wawili wakati wa kampeni ilikuwa ya kumbwaga aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo katika kiny’ang’anyiro cha pamoja.

Bw Oduol amewahi kuwania ugavana 2013 na katika uchaguzi mdogo wa 2014 na 2017 ambapo alimtoa kijasho Gavana wa kwanza Cornell Rasanga.

Pengine sasa amegutuka kujiona mbabe huku akiona kiti cha unaibu gavana kama kidogo na hawezi kufuata amri ya Bw Orengo. Isitoshe, Bw Oduol anatoka eneobunge la Alego Usonga ambalo lina wapigakura wengi zaidi Siaya.

Kutokana na hilo anaona kana kwamba mchango wake kwenye uongozi wa kaunti hauthaminiwi ilhali alileta kura nyingi kapuni.

Ili kutatua suala hili, Kinara wa ODM Raila Odinga anastahili kuingilia kati na kuwapatanisha wanasiasa hawa wawili. Siaya bado ipo nyuma kimaendeleo kutokana na uliokuwa uongozi duni wa Bw Cornel Rasanga.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ammegea Echesa mnofu serikalini

Kipchoge azoa Sh7.4 milioni za tuzo ya Kihispania ya Binti...

T L