NA CECIL ODONGO
KINARA wa Azimio la Umoja Raila Odinga anapasa kukoma kuwachezea shere wafuasi wake kila mara kwa kuchukua mkondo wa siasa ambao unawaacha na maswali mengi bila majibu.
Mnamo Jumapili jioni, kiongozi huyo wa ODM pamoja na vinara wengine wa muungano huo walisitisha maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini.
Lengo kuu la maandamano hayo ambayo yalikuwa yakifanyika kila Jumatatu na Alhamisi liilikuwa kupigania gharama ya maisha irudi chini. Kati ya sababu nyingine pia alizotaja Raila ni kurejeshwa kazini kwa Makamishina waasi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC), kufunguliwa mwa mitambo ya IEBC ili ukweli ufahamike kuhusu uchaguzi mkuu uliopita na kupinga asasi za serikali kutekwa na afisi ya Rais.
Bw Odinga alisitisha maandamano hayo baada ya Rais William Ruto kumrai afanye hivyo ili baadhi ya masuala ambayo anayoyapigania hasa uteuzi wa makamishina wapya wa IEBC yatatuliwe na mabunge ya seneti na kitaifa. Kabla ya kusitisha maandamano hayo, yalikuwa yamefanyika mara tatu katika maeneo mbalimbali hasa katika miji ya Kisumu na Nairobi.
Vifo vilitokea kikiwemo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maseno. Pia wafanyabiashara walikuwa wamepata hasara nyingi kwa kutatizika kuendelea na shughuli zao kila siku. Inasikitisha kwamba, Raila anauchukulia uungwaji mkono wa wafuasi wake hivi hivi tu bila kuzingatia jinsi wanavyojinyima mengi na kuhatarisha maisha yao wakimpigania apate haki.
Ni dhahiri kuwa hakuna chochote alichopata au atakachoambulia baada ya kuwaongoza watu kuandamana ambapo hasara nyingi imetokea pamoja na vifo. Je, mitambo ya IEBC itafunguliwa na ukweli kuhusu uchaguzi mkuu uliopita kubainika? Na inakuaje bei ya unga ambayo bado ipo juu pamoja na gharama ya maisha? Je, huo mchakato bungeni utawarejesha Juliana Cherera na wenzake ambao Bw Odinga alikuwa akiwapigania kazini? Kuna baadhi ya wanasiasa ambao walijiunga na mrengo wa Kenya Kwanza kutoka ngome ya Bw Odinga ya Nyanza. Wafuasi wa ODM wamekuwa wakiwarejelewa kama wasaliti na wenye njaa huku wakisisitiza kwamba hawafai kusikizwa na raia.
Je, hii hatua ya Raila kuanza ukuruba na Rais William Ruto ina tofauti gani na wanasiasa hao waasi ambao baadhi yao wameshapokezwa nyadhifa kama mawaziri wasaidizi? Suala kuu ambalo Raila alikuwa akipigania ni haki kuhusu uchaguzi mkuu uliopita na wafuasi wake waliamini kwamba ukweli ungefahamika lakini wapi?