• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
CECIL ODONGO: Ruto, Moi wasihadae wahanga wa Mau wakijitafutia kura za uchaguzi ujao

CECIL ODONGO: Ruto, Moi wasihadae wahanga wa Mau wakijitafutia kura za uchaguzi ujao

Na CECIL ODONGO

INASIKITISHA kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi sasa wanalitumia suala la msitu wa Mau kwa manufaa yao ya kisiasa huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

Mahangaiko ya watu ambao walifurushwa msituni humo yamekuwa yakiendelea miaka nenda miaka rudi na hayafai kutumiwa kusaka kura na wanasiasa wenye mazoea ya kufanya hivyo kisha kutokomea baada ya kupigiwa kura.Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013, Dkt Ruto alitumia suala hilo kujikweza zaidi kisiasa kama kigogo wa Wakalenjin wakati ambapo Kinara wa ODM Raila Odinga naye alikuwa akiongoza juhudi za kuokoa msitu huo.

Wakati huo, Dkt Ruto na viongozi wa jamii ya Kalenjin, walimpinga Bw Odinga na kudai kuwa alikuwa akitumia suala hilo kudhulumu jamii hiyo ilhali ilimpigia kura kwa wingi mnamo 2007.Pamoja na Rais Kenyatta ambaye wakati huo alikuwa Naibu Waziri Mkuu, waliandaa mchango wa kuwasaidia wahanga hao na hadi leo haifahamiki iwapo msaada huo uliwafikia watu lengwa na iwapo walioondolewa mwanzoni walipata makao mapya.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga aliyeungwa mkono na vigogo wa jamii ya Maasai wakiongozwa na aliyekuwa waziri William Ole Ntimama alikosa kura za jamii hiyo huku suala hilo likiwa kati ya yaliochangia kulemewa kwake uchaguzi wa 2013.

Baada ya kufikia malengo yao na kuingia uongozini, Dkt Ruto aliwasahau wahanga hao na hata hakutamka lolote wakati ambapo watu waliosalia msituni walifurushwa kwa mara nyingine 2019.Inashangaza kuwa wiki jana, Dkt Ruto ambaye alikuwa ziara ya kampeni Narok aligeuka na kusema aliunga mkono kuondolewa kwa watu msituni, tamko hilo likilenga kushawishi jamii ya Maasai impigie kura 2022.

Bw Moi pia alitembelea Mau na kusema kuwa atahakikisha wanaoishi kando ya barabara, wanapata ardhi mbadala na makao. mapya kabla ya uchaguzi mkuu ujao.Je, amekuwa wapi muda huu wote ambapo familia zilizoondolewa msituni zimekuwa zikiteseka?

Na ikiwa imesalia miezi minane kabla ya uchaguzi mkuu uandaliwe, kuna hakikisho gani kuwa mchakato wote wa kupata ardhi na kuwapa watu hawa makao utafanikishwa?Huenda hii ni mbinu nyingine ya Dkt Ruto na Bw Moi kusaka uungwaji mkono kisha baada ya kura watokomee huku wakiwaacha wahanga wa Mau wakiteseka wakisubiri uchaguzi mwingine.

You can share this post!

Helikopta kutumika Mama Lucy mwakani kutoa huduma- NMS

Ufisadi: EACC yataka KPA ichukuliwe hatua

T L