• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
CECIL ODONGO: Viongozi wa ODM walioenda Ikulu ni wasaliti, wanafiki na wanadharau Raila

CECIL ODONGO: Viongozi wa ODM walioenda Ikulu ni wasaliti, wanafiki na wanadharau Raila

NA CECIL ODONGO

HATUA ya baadhi ya wabunge wa ODM kwenda Ikulu ni usaliti mkubwa na dharau kwa kiongozi wa chama chao, Bw Raila Odinga.

Wabunge hao Mark Nyamita (Uriri), Phelix Odiwuor Jalang’o ( Lang’ata), Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Ochieng’ ( Gem), Caroli Omondi (Suba Kusini), Walter Owino ( Awendo), Paul Abuor (Rongo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda, walifika Ikulu mnamo Jumanne kukutana na Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Hata hivyo, ni ucheshi kwao kudai walienda kufuatilia hali ya miradi ambayo Rais Ruto alizindua alipozuru Nyanza mwezi Januari.

Cha kusikitisha ni wao kudai kwamba walifanya hivyo baada ya kuhofia utawala wa Kenya Kwanza ungesitisha miradi hiyo, kutokana na shinikizo zinazoendelezwa kwa sasa na Bw Odinga dhidi ya serikali.

Mwanzo, wanasiasa hawa huenda ni zumbukuku kudai wanahofia miradi hiyo haingetekelezwa kwa sababu za kisiasa.

Eneo la Nyanza au ngome za kisiasa za Bw Odinga ni sehemu ya Kenya, na wakazi wake wanalipa ushuru kama Wakenya wengine.

Hivyo, wao kupata maendeleo si kwa hisani ya Rais au wakuu serikalini jinsi ilivyokuwa enzi za Kanu.

Pili, ni usaliti mkubwa wakati huu Bw Odinga anaendeleza shinikizo dhidi ya serikali kutokana na kile amedai ni kupokonywa ushindi wake, kwa wabunge wanaostahili kusimama naye kumtoroka.

Wabunge hao wana vyeo kwa hisani ya ODM, Bw Odinga na wakazi wa maeneo yao ambako kinara huyo ana ufuasi mkubwa.

Walichaguliwa si kwa umaarufu wao bali ushawishi wa Bw Odinga na ODM miongoni mwa wakazi wa maeneo yao.

Wangekuwa wakweli kuhusu ziara yao Ikulu wangeshauriana na kigogo wa chama chao kwanza.

Huu si unafiki tu bali unaibua madai kuwa walifanya hivyo kutimiza maslahi yao ya kibinafsi badala ya kujitetea eti walienda kusaka hakikisho kuhusu miradi ya maendeleo.

Kutokana na tukio hili, huenda wanasiasa hawa wamejiangamiza kwa kuwa sasa wanatazamwa kama waasi na wasaliti hasa katika jamii yao.

Rais Ruto alipokuja Nyanza alilakiwa karibu na viongozi wote wa ODM. Kwa nini hawa walijiteua na kufika ikulu kisha wengine wakaachwa nje?

Mara nyingi hata Kiafrika jamii inapoenda vita basi huwa kuna umoja na mashauriano kabla ya uamuzi wowote kufanyika.

Wakati huu wangeungana na viongozi wa ODM na wengine wa Azimio la Umoja katika juhudi hizi ambazo zimekuwa zikirejelewa kama za ukombozi.

Wabunge hawa wanashikilia vyeo vyao kwa hisani ya ODM, Bw Odinga na wakazi wa maeneo wanatoka ambako waziri huyo ana ufuasi mkubwa.

Ukweli ni kuwa walichaguliwa si kutokana na umaarufu wao bali kutokana na ushawishi wa Raila na umaarufu wa ODM miongoni mwa wakazi wa maeneo yao.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Licha ya misukosuko Afrika ni bara lenye...

Maswali kuhusu tukio la uvamizi kwa Matiang’i

T L