NA CHARLES WASONGA
TANGU walipongia mamlakani Septemba 13 mwaka jana, Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua wamekuwa wakihudhuria ibada za kutoa shukrani kwa Mungu kwa ushindi wao.
Ni vizuri viongozi wetu kumcha Mungu kila mara kwani kufanya hivyo watapata baraka za Maulana kuendesha vyema majukumu yao ya serikali.
Hata hivyo, Rais Ruto, Bw Gachagua na viongozi wengine wanaoandamana nao katika maeneo hayo ya kuabudu wanafaa kuhubiri amani na maridhiano, hususan miongoni mwa wanasiasa na wananchi.
Inavunja moyo kuona siasa ndizo hushamiri katika mikutano hiyo ya maombi badala ya jumbe za kupalilia mazingira ya utulivu yatakayowezesha serikali kutekeleza ahadi chungu nzima walizotoa wakati wa kampeni.
Rais Ruto na Bw Gachagua wamegeuza mikutano hiyo kama majukwaa ya kujibu makombora ambayo kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga hutupa katika mikutano yake ya kupinga utendakazi duni wa Kenya Kwanza.
Isitoshe, Dkt Ruto hutumia madhabahu ya makanisa kuchapa siasa za kumshambulia kinara huyo wa Azimio, ambaye naye amepata msukumo hata zaidi kukosa serikali.
Rais Ruto na wanasiasa wengine waheshimu maeneo ya kuabudu na wakome kuyatumia kuendeleza malumbano kati yao na viongozi wa upinzani.
Maabada ni maeneo matakatifu ambako watu huenda kupata lishe ya roho sio siasa. Kimsingi, mikutano hiyo inapasa kuongozwa na viongozi wa kidini wala si wanasiasa.
Kwa mfano, katika mkutano uliofanyika mjini Nakuru, Rais Ruto alitetea wabunge wa Jubilee na ODM ambao wametangaza kuunga mkono serikali yake ndani na nje ya Bunge.
Naye Bw Gachagua alitumia muda mwingi kumshutumu aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kwa kudai maafisa walivamia nyumba yake wiki jana ili kumkamata.
Je, mkutano huo ulikuwa wa maombi au wa kupiga siasa?