• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
CHARLES WASONGA: Serikali ifanikishe azma ya afya kwa wote ili raia wanufaike kimaendeleo

CHARLES WASONGA: Serikali ifanikishe azma ya afya kwa wote ili raia wanufaike kimaendeleo

NA CHARLES WASONGA

MNAMO Septemba 2020, mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) yalipitisha muafaka kuhusu Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) chini ya kauli mbiu: “Kuungana kujenga ulimwengu wenye afya bora.”

Kenya ni mojawapo ya mataifa wanachama wa umoja huo. Muafaka huu ulilenga kuthibitisha kuwa UHC ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Chini ya mpango huo angalau watu bilioni moja kote dunia wanapaswa kupokea huduma toshelezi za afya, na kwa gharama nafuu, kufikia mwaka wa 2023.

Humu nchini, serikali ya Kenya Kwanza, sawa na ile ya Jubilee iliyoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, imeorodhesha afya kwa wote kama mojawapo wa agenda kuu ambazo inapania kutimiza.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwengu (WHO), gharama ya juu ya matibabu katika mataifa ambako idadi kubwa ya watu ni wenye mapato ya kadri, kama vile Kenya, ni kikwazo kikuu katika uafikiaji wa mpango wa afya kwa wote.

Hii ndiyo maana serikali hii Rais William Ruto haina budi kuhakikisha kuwa imefanikisha ajenda ya afya kwa wote kwa kutumiza ahadi yake ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi anasajiliwa na Bima ya Kitaifa ya Hazina ya Matibabu (NHIF).

Wale ambao hawawezi kumudu kulipa michango ya kila mwezi kwa hazina hiyo walipiwe na serikali, alivyoahidi Dkt Ruto wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Hii ni kwa sababu, kulingana na takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) Wakenya 23.4 milioni walikuwa ni masikini hohehahe mwaka wa 2020.

Bila shaka kufikia sasa idadi hii imeongezeka kutokana na changamoto za kiuchumi zinazoizonga Kenya na ulimwengu kwa ujumla.

Hii ndiyo maana japo pendekezo la kupunguzwa kwa ada ya NHIF kwa watu wenye mapato ya chini hadi Sh200 kutoka Sh500 kila mwezi linafaa, bado serikali inayo wajibu wa kugharimia matibabu ya wale wasiojiweza kabisa.

Aidha, ili kufanikisha mpango huu wa UHC, serikali kuu kwa ushirikiano na zile za kaunti zizuie uwezekano wowote wa kutokea kwa migomo ya wahudumu wa afya.

Aidha, serikali ihakikishe kuwa hospitali za umma zina dawa, vifaa vya kimatibabu na mitambo hitaji ya kusaidia katibu magonjwa sugu ili Wakenya wasiende ng’ambo kusaka matibabu.

Inaridhisha kuwa juzi, Rais Ruto alikariri kuwa serikali yake imejitolea kuelekeza rasilimali nyingi katika sekta ya afya kukabiliana na changamoto zinazokabiliwa sekta hiyo.

“Familia nyingi kote nchini zimezongwa na mzigo mzito wa kugharamia bili za matibabu kutokana na ukosefu wa ajira, kati ya changamoto zingine. Kama serikali ya kitaifa, tutasaidia kuwa kutenga fedha zaidi katika sekta ya afya,” Rais akasema mwezi Aprili alipoongoza hafla ya ufunguzi wa hospitali AAR katika Kiambu Road, Nairobi.

Ukweli ni kwamba serikali haiwezi kufikia malengo yake ya maendeleo raia wengi wanazongwa na matatizo ya kiafya.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Kwanza kwa Azimio: Msije meza ya mazungumzo na...

Mbunge aliyeonyesha chuki kwa Hayati Mzee Jomo Kenyatta...

T L