• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:00 AM
CHARLES WASONGA: Serikali, maafisa wa polisi wasivuruge maandamano yajayo ya Azimio

CHARLES WASONGA: Serikali, maafisa wa polisi wasivuruge maandamano yajayo ya Azimio

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI isiingilie maandamano ambayo yameitishwa na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kuanzia Mei 02, 2023.

Imebainika kuwa fujo, uharibifu wa mali na hata maafa yalitokea katika awamu ya kwanza ya maandamano baada ya polisi kutumwa kutawanya waandamanaji.

Kwa mfano, kabla ya msururu wa maandamano yaliyoanza Machi 20 siku za Jumatatu na Alhamisi, wafuasi wa Azimio waliandamana mjini Kisumu kwa amani. Fujo hazikushuhudiwa sababu maafisa wa polisi hawakutumwa kutawanya wafuasi hao wa kinara wa Azimio, Bw Raila Odinga. Kando na hayo, tangu Desemba iliyopita viongozi wa muungano huo wamehutubia zaidi ya mikutano 17 ya hadhara katika miji mbalimbali nchini pasina fujo kushuhudiwa.

Wiki jana, mkutano wa Azimio ulianza na kuisha kwa amani mjini Murang’a. Hii ni licha ya kwamba, awali polisi walitaja mkutano huo kama haramu na wakakataa kutoa kibali kwa waandalizi wakiongozwa na aliyekuwa Gavana Mwangi wa Iria wa Murang’a.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa polisi Murang’a walipokea agizo kutoka kwa wakuu wao kutoingilia mkutano huo “ili kuzuia machafuko na uharibifu wa mali.”

Hii inamaanisha wakuu hao imewapambazukia kwamba chanzo cha machafuko katika mikutano au maandamano ya Azimio huwa ni jaribio lao la kuivunjilisa mbali. Wakuu hao pia wanafaa kushauri polisi kutoingilia maandamano ambayo Azimio wamepanga kurejelea kuanzia Mei 2.

Serikali iige mfano wa Afrika Kusini ambako polisi wamekuwa wakitoa ulinzi kwa wafuasi wa upinzani wakiongozwa na Julius Malema kwenye maandamano yao. Kwa upande wao, Bw Odinga na vigogo wenzake wa Azimio washauri wafuasi wao kudumisha amani wanapoandamana. Wahalifu ambao wanapenyeza katika maandamano kupora mali ya watu wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Ruto aondoe Keynan kamati ya mazungumzo na...

TAHARIRI: Nguzo kuu ya dini ni utu bali si maisha ya baada...

T L