• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
CHARLES WASONGA: Uchunguzi wa seneti kuhusu bei ya umeme haufai, Ruto ndiye mwenye suluhu

CHARLES WASONGA: Uchunguzi wa seneti kuhusu bei ya umeme haufai, Ruto ndiye mwenye suluhu

NA CHARLES WASONGA

MNAMO Jumatano wiki hii, Bunge la Seneti lilianza kuchunguza zabuni tata ambazo zilitiwa saini na kampuni za kibinafsi za kuzalisha umeme (IPPs) ili kuiuzia umeme kampuni ya umeme nchini (KPLC).

Uchunguzi huo unaoendeshwa na Kamati ya Seneti kuhusu Kawi unajiri wakati ambapo bei ya umeme imepanda kwa asilimia 10 kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na kudorora kwa thamani ya Shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kimataifa.

Taswira ya kupotosha inayojitokeza hapa ni kwamba zabuni hizi tata ndizo sababu kuu ya kupanda kwa bei ya sumeme. Hiyo sio kweli. Ikumbukweli kwamba mapema mwezi huu Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) ilipandisha ada inayotozwa bei ya umeme, kutokana na kupanda kwa bei mafuta, hadi Sh8.3 kwa kipimo kimoja cha umeme ambacho kilikuwa kinatozwa Sh6.59 mnamo Februari.

Epra pia imepandisha tozo za ubadilishanaji wa sarafu dhidi ya Dola ya Amerika hadi Sh2.16 kwa kila kipimo cha umeme kutoka Sh1.85 mwezi Februari.
Hii ni kutokana na kudorora kwa thamani ya Shilingi ambayo sasa inabadilishwa kwa Sh128 dhidi ya Dola.

Hatua hii imechangia kupanda kwa bei ya umeme kwa wateja wa kawaida kutoka Sh22 kwa kipimo hadi Sh20 iliyotozwa mwezi Februari. Lakini tukumbuke kuwa Rais William Ruto mwenyewe alitangaza kuwa serikali yake kamwe haitaongeza bei ya umeme kama sehemu ya mpango wake wa kupunguza gharama ya maisha. Kinaya ni kwamba mnamo Septemba 13, 2022, Dkt Ruto mwenyewe aliondoa ruzuku kwa bei ya umeme; iliyowekwa na mtangulizi wake, Bw Uhuru Kenyatta.

Alitetea hatua hiyo akisema kuwa kufuatia hatua hiyo, pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya bei ya unga, serikali iliweza kuokoa Sh25 bilioni.

Kwa hivyo, sioni haja ya Kamati hiyo ya Seneti inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga, kuchunguza kandarasi kati ya IPPs na KPLC ilhali serikali ya Rais Ruto ina uwezo wa kushughulikia suala hilo kwa wepesi mno.

Ninakumbuka kuwa katika bunge la 12, kamati hiyo hiyo ikiongozwa na mtangulizi wa Bw Wamatinga, Ephraim Maina, lilichunguza zabuni hizo na kuandaa ripoti. Ripoti hiyo ingali katika seneti.

Kwa hivyo, badala ya kuanzisha uchunguzi mpya, ninadhani Kamati ya Wamatinga ingetumia ripoti iliyoandaliwa na Bw Maina.

  • Tags

You can share this post!

Waboni walia kupuuzwa katika umiliki wa ardhi

Kioni ashtakiwa kwa kudai Raila ndiye alishinda urais

T L