• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
CHARLES WASONGA: Vikwazo viondolewe kabla ya vitambulisho vipya kutolewa

CHARLES WASONGA: Vikwazo viondolewe kabla ya vitambulisho vipya kutolewa

NA CHARLES WASONGA

MPANGO wa serikali wa kuanzisha vitambulisho vya kitaifa vya kidijitali kufikia mwishoni mwa mwaka huu ni mzuri ila unapasa kuendeshwa kwa uangalifu mkubwa.

Hii ni kwa sababu maelezo yote ya kila Mkenya yatahifadhiwa kwenye sajili moja hali ambayo itawawezesha kupokea huduma za serikali kwa urahisi.

Matumizi ya vitambulisho hivyo vya kidijitali pia yataiwezesha serikali kuendesha vizuri mipango ya ugavi wa rasilimali kwa manufaa ya Wakenya.

Isitoshe, chini ya mfumo huu, watoto waliozaliwa nchini watapewa Nambari Maalum ya Utambulisho (UPI Number) itakayoisadia serikali kupanga namna ya kuwapa huduma za kimsingi kama elimu na afya.

Lakini maswali mengi yanaibuliwa kuhusu mpango huu mpya ikizingatiwa kuwa mpango wa awali wa usajili wa Wakenya kwa mfumo uu huu wa kidijitali ulifeli.

Jumla ya Wakenya 7.3 milioni walisajiliwa kwa mfumo huo na wakapewa kadi za Huduma Namba; walizotarajiwa kutumia kupata huduma za serikali haraka badala ya kutumia vitambulisho vya kitaifa.

Aidha, kadi hizo zingetumika mahala pa kadi za Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF), Paspoti, Cheti cha Kuzaliwa, Leseni ya Uendeshaji magari miongoni mwa stakabadhi nyingine za huduma.

Lakini mpango huo ambao ulianzishwa Mei 15, 2019 ulisitishwa baada ya Mahakama Kuu kuamua kwamba ulikiuka Katiba. Ilidaiwa kuwa serikali haikuweka mikakati thabiti ya kulinda data za siri za Wakenya, kinyume na hitaji la Katiba kuhusu usiri wa maelezo ya kibinafsi ya mtu.

Isitoshe, mpango huo uliingizwa siasa baada ya mrengo wa chama cha Jubilee ulioongozwa wakati huo na Rais William Ruto (akiwa Naibu Rais) kudai serikali ilipania kutumia mpango huo wa Huduma Namba kufanikisha wizi wa kura kwa manufaa wa kiongozi wa Azimio, Raila Odinga. Bw Odinga, ambaye pia ni kiongozi wa ODM, alikuwa akiungwa mkono na Rais wa wakati huo, Bw Uhuru Kenyatta, ambaye sasa amestaafu.

Kilichowaudhi Wakenya zaidi ni kwamba mpango huo ulisitishwa baada ya kufyonza Sh10.6 bilioni, pesa ambazo zingeokolewa ikiwa serikali ingejipanga vizuri kabla ya kuanzisha mpango huo. Hii ndio maana ni jambo la busara kwa serikali kuweka maandalizi madhubuti kabla ya kuanzisha mpango huo wa usajili wa Wakenya kwa ajili ya kupewa vitambulisho vipya vya kitaifa vya kidijitali.

Kwa mfano, serikali hii ya Kenya Kwanza ihakikishe kuwa imeondoa vikwazo vyote vya kisheria ambavyo vinaweza kuhujumu mpango huu, ambao yamkini una malengo mazuri. Hii itawezekana tu ikiwa Serikali Kuu, kupitia afisi za Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa, itarejesha bungeni Mswada wa Huduma nambari 57 wa 2021.

  • Tags

You can share this post!

Raila atabasamu korti ikizaba Ruto

Haji sasa atetewa na wabunge kutoka jamii za wafugaji

T L