• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
CHARLES WASONGA: Wengi kutoka familia maskini watakosa ufadhili wa masomo

CHARLES WASONGA: Wengi kutoka familia maskini watakosa ufadhili wa masomo

NA CHARLES WASONGA

SASA imebainika kuwa huenda wanafunzi wengi kutoka familia maskini walioitiwa fursa za kujiunga na vyuo vikuu vya umma wakakosa ufadhili kutoka kwa serikali chini ya mfumo mpya wa ufadhili wa masomo ya juu.

Hii ni kwa sababu chini ya mfumo huu, serikali imeamua kutumia maafisa wa utawala (baadhi yao waliokosa maadili) kubaini wanafunzi watakaofaulu kupewa misaada ya masomo (scholarship), mikopo na basari.

Wanafunzi wenye mahitaji wameshauriwa kutuma maombi ya aina hizi za ufadhili kufikia Agosti 27, 2023. Kisha wanatarajiwa kuripoti vyuoni kuanzia mwezi ujao wa Septemba.

Inasemekana kuwa kiwango cha ufadhili ambacho kila mwanafunzi atapata kitaamuliwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vitakavyowekwa na Bodi ya Kufadhili Elimu ya Juu (HELB) na Hazina ya Vyuo Vikuu (UF).

Wazazi wengi bado hawafahamu baadhi ya vigezo kando na matumizi ya machifu na manaibu wao. Kinachojulikana ni kwamba si wanafunzi wote waliotuma maombi watafaulu kupata mikopo, misaada ya masomo au basari.

Mwezi jana, walimkabili Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu, na msururu wa maswali kuhusu suala, haswa vigezo vitakavyotumiwa kubaini uhitaji wa wanafunzi.

Waziri alisema kuwa chini ya mfumo huu, wanafunzi mayatima watapewa asilimia 82 ya karo kwa njia ya msaada wa masomo na asilimia 18 kama mkopo.

Wanafunzi kutoka familia masikini nao watapewa msaada wa masomo wa kima cha asilimia 70 ya karo na kupewa mkopo wa HELB wa kima cha asilimia 30.

Wale walioko katika kategoria ya uhitaji wa wastani watapewa msaada wa masomo kima cha asilimia 53 na mkopo wa hadi asilimia 40 ya karo.

Aidha, Bw Machogu alisema kuwa wanafunzi wenye uhitaji mdogo watapewa msaada wa masomo wa kima cha asilimia 38 na mkopo wa hadi asilimia 55 ya karo kila mwaka.

Waziri alikariri kuwa si lazima kwa wanafunzi katika kategoria hizi za uhitaji wapate viwango hivyo vya misaada ya masomo, mikopo au basari.

Bw Machogu aliwakasirisha wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Elimu aliposema kuwa serikali itatumia maafisa wa utawala, haswa machifu na manaibu wake kubaini viwango vya uhitaji wa wanafunzi.

Alisema kuwa ripoti kutoka maafisa hawa wa utawala ndio itatumiwa na serikali kukadiria viwango vya ufadhili kwa kila mwanafunzi wa vyuo vikuu.

Fasiri yangu ni kwamba chini ya mfumo huu wanafunzi wengi kutoka familia masikini watakosa ufadhili wa serikali kwani ni wazi baadhi ya machifu wataitisha hongo kupendekeza wanaopasa kufaidi.

Tumewaona machifu hawa na manaibu wao washiriki uovu huu nyakati za usajiliwa wa wakulima kwa mpango wa utoaji mbolea ya bei nafuu, usambazaji wa chakula cha msaada kati ya mipango mingine ya kusaidia wenye mahitaji mbalimbali katika jamii.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wasaka mshukiwa anayetembea akiwa amejihami kwa shoka

Tanzia: Olesia wa Kenya Lionesses aaga dunia

T L