• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
DOUGLAS MUTUA: Kweli Kenya imehalalisha ushoga au ni hisia kali tu?

DOUGLAS MUTUA: Kweli Kenya imehalalisha ushoga au ni hisia kali tu?

NA DOUGLAS MUTUA

HIVI haramu imehalalishwa, yaani ushoga ukaidhinishwa kisheria nchini Kenya?

Hii ninayosikia ni mihemko ya kawaida tu au watu wanakifahamu fika wanachokisema?

Tuelewane tangu mwanzo: Binafsi ni mhafidhina, hivyo ninaupinga ushoga – usagaji na ubasha – kwa asilimia zote na sitabadili msimamo huu hadi nifukiwe kaburini.

Hata hivyo utaniwia radhi, lazima nikwambie hivi: kuna dhana za kiusomi ambazo mtu wa kawaida hawezi kuzielewa, ila analazimika kuishi nazo kwa kuwa zinamwathiri moja kwa moja na haziepukiki.

Kwa neno usomi hapa narejelea ubobevu wa mtu katika fani fulani, si umiliki wa stakabadhi za kuketi darasani na kuweza kukariri vitabu kadhaa kisha akapita mtihani.

Mathalan, dhana kwamba mtu hahukumiki hadi atakapokutwa na hatia baada ya kesi yake kusikilizwa kikamilifu haiingii akilini mwa kila mtu.
Ni kwa mintaarafu hii ambapo utawasikia makabwela wakisema anayeua naye auawe, kisasi kilipwe papo hapo.

Na watetezi wa haki za binadamu wakisisitiza mkondo mzima wa sheria ufuatwe wanaambiwa wangemwambia mapema muuaji huyo kwamba kuua mtu ni kumvunjia haki ya kimsingi.

Ni watu wasioelewa dhana hiyo ambao watapata mshtuko wa moyo wakisikia mshtakiwa wa mauaji, ikiwa hana uwezo wa kifedha, anatafutiwa wakili na serikali, tena inamlipia huduma hiyo.

Ngoja wasikie kila mshtsakiwa wa mauaji ni sharti afanyiwe vipimo ili ibainike iwapo ana akili timamu! Hapo ndipo wanapodai visingizio vya kumwondolea mshtakiwa hatia vinatafutwa.

Wapenzi wa mashairi ya Kiswahili, hasa tunaojiita wanamapokeo, huchukulia kuwa najis ushairi huru unaoandikwa bila kuzingatia kanuni zozote, ila wakiwa wasomi wanauvumilia.

Usomi unakupanua mawazo na kukusadikisha kwamba huna ukiritimba wowote; dunia imejaa watu wasiokubaliana na mawazo yako hata ikiwa unadhani yako sahihi kiasi gani.

Dhana hii inanikumbusha miaka mingi iliyopita, nikiwa bado na makeke ya ujana, ambapo marehemu Prof Ken Walibora aliniomba nimpe mashairi ya masuala-ibuka ili achapishe diwani.

Nililotunga kwa kujiaminia kabisa liliitwa ‘Madhabahu ya Mabasha’, nikiwasuta wanaume waliooana. Ken hakuligusa, wala hakutaka tulijadili!

Ingawa ningali na uhafidhina wangu na ushoga unanipa kinyaa, ninapolisoma shairi hilo natambua nilivyokuwa na mawazo finyu, tena ninamwelewa mhafidhina mwenzangu Ken na usomi wake wa kuheshimu misimamo ya watu asiokubaliana nao.

Dhana ya Katiba ya kupinga ubaguzi wa aina yoyote ule, ambayo imetumiwa na majaji wa Mahakama ya Upeo ya Kenya kuwapa mashoga uhuru wa kutangamana, haieleweki na kila mtu.

Haiwakilishi misimamo binafsi ya majaji wa mahakama hiyo bali ni sauti ya Katiba tu ilivyoandikwa. Tukitaka kuzuia maamuzi ya aina hiyo, basi na tuhalalishe ubaguzi!

Kudai majaji hao wamelipwa ili wafanye maamuzi hayo ni kufichua ufinyu wa mawazo yako; baadhi yao ni wahafidhina ila wamebanwa na Katiba wakaamua wasiyokubaliana nayo.

Raha ya usomi ni kwamba hata dhana isiyokukaa vizuri kama bingwa wa fani husika, mradi ina mizizi na ithibati za kisheria na kiusomi, inauzidi nguvu mtazamo wako binafsi.

Linalonikosesha usingizi ni kwamba uamuzi huo unapingwa na watu wengi wasiofanya chochote kupalilia maadili ya Kiafrika, lao kuu ni kufoka tu.

Hawajui makuzi ya watoto wao yakoje: Shamba-boi anawafundisha wanao mambo yepi akienda nao malishoni? Yaya naye anaigiza ya unyagoni na mabinti zako ukimwacha nao kutwa nzima?

Naamini ushoga ni utundu kwa kuwa hakuna ithibati ya kisayansi kwamba watu huzaliwa nao, ni tabia mbovu inayotokana na mazoea ya maovu, iwe kwa hiari au shuruti.

Mbinu bora ya kuukabili si kuulaani tu, huko kunauvumisha zaidi. Upesi peleka watoto kanisani na misikitini wangali wachanga, wakirejea kaa nao uwafunze maadili na mienendo ya kwenu.

Hakikisha unajua watu wanaotangamana nao; usikubali mwanao aende faraghani peke yake na mtu asiye mzazi wake.

Ni vigumu, lakini inabidi kwa kuwa dunia imebadilika. Mashoga wanasajili wafuasi, ni juu yako nami tuhakikishe hawafanikiwi kamwe.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kaunti yafadhili 300 kuhudhuria mazishi ya mzee wa jamii ya...

WANDERI KAMAU: Nigeria ni mfano bora kuwa mtu mui hatimaye...

T L