• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
DOUGLAS MUTUA: Maadili yataamua ufanisi au kuporomoka kwa Nigeria

DOUGLAS MUTUA: Maadili yataamua ufanisi au kuporomoka kwa Nigeria

NA DOUGLAS MUTUA

TAIFA la Nigeria linapiga chafya leo, tahadhari usipate mafua!

Hivi uchaguzi wa urais unaofanyika leo nchini humo utawaathiri vipi Waafrika wengine?

Kipo kichekesho ambacho kila nikikisikia, nusra kinitegue mbavu. Kinahusu idadi ya watu nchini Nigeria. Inaaminika taifa hilo ndilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Hata hivyo, wazushi hukaa na kuuliza: aliyewahesabu ni nani? Kimsingi, swali hilo linaashiria kuwa Mnigeria haaminiki, eti huenda aliongeza idadi hiyo. Tunaoishi ughaibuni tuna mashaka sana kila tunapohusiana na watu wa taifa hilo kwa kuwa mara nyingi utawapata kwenye sakata za kila aina, hasa za kughushi stakabadhi.

Wengi wao huwa na pasipoti tatu za mataifa mbalimbali, isipokuwa taifa lao wenyewe! Mnigeria wa kawaida atakuwa na pasipoti ya Ghana, Afrika Kusini na taifa jingine. Kisa na maana, wanajaribu kukimbia sifa mbaya zinazonasibishwa na taifa lao: utakatishaji pesa, kughishi stakabadhi, ulanguzi wa dawa za kulevya na kadhalika.

Ni kwa mitaarafu hiyo ambapo tunatahadharishana kiutani kwamba ikiwa unasafiri kwa ndege, wakati wa ukaguzi wa kiusalama, hakikisha humkaribii Mnigeria kwenye foleni.

Kwani kuna nini? Raia wa nchi hiyo na watu wengine wanaowakaribia kwenye foleni mara nyingi hukaguliwa kupita kiasi, wakati mwingine hulazimishwa kuvua nguo zote katika shughuli hiyo.

Hayo yanasikika kama maonevu dhidi ya raia wa taifa zima, lakini ukweli ni kwamba yanaendelea kila siku, na hakuna anayethubutu kulalamika ili asiwekwe katika orodha ya wasafiri hatari kama Miguna Miguna!

Matatizo ya Nigeria yanapaswa kumpa hofu kila mtu, hasa Mwafrika, kwa kuwa idadi ya raia wa taifa hilo ni kubwa, tena wapo kila mahali. Wamewekeza mabilioni ya fedha katika kila nchi barani Afrika, hivyo ushawishi wao upo kotekote. Wana nyumba za kupangisha nchini Kenya, wanauza dawa za kulevya, wanasumbua kwenye vilabu vya starehe, huwakosi mtandaoni na kadhalika.

Kwamba taifa hilo linafanya uchaguzi wa urais leo ni suala la kumvutia na kumshughulisha kila Mwafrika kwa kuwa matokeo ya shughuli hiyo yatakuwa na athari fulani.

Kimataifa, Nigeria haiwezi kupuuzwa. Hata mataifa makuu yanaiogopa kwa kiasi fulani kwa kuwa na sera zisizombembeleza yeyote asiyewaheshimu Wanigeria.

Kwanza, Nigeria haina kiasi kimoja cha ada inayotozwa watu wanaoomba visa ya kusafiria kulizuru taifa hilo. Ada inayotozwa ili kupata visa ya kuzuru Nigeria hutegemea ada ambayo taifa lako linawatoza raia wa Nigeria wanaotaka kuzuru kwenu.

Mathalan, ikiwa Kenya inatoza raia wa Nigeria Sh10,000, Mkenya anayetaka kwenda Nigeria atalazimika kulipa kiasi sawa na hicho, lau sivyo ajikalie kwao!

Sera nyingine ambayo inawashangaza wengi inahusiana na uhamiaji. Taifa lolote linalothubutu kumfukuza raia wa Nigeria linapaswa kujiandalia mrejesho usio mwema.

Kenya ilitambua ukweli huu ilipomweka ndani ya ndege na kumrejesha Nigeria, Bw Anthony Chinedu, aliyeshukiwa kuwa mlanguzi wa dawa za kulevya.

Ndege ya kukodi aliyorejeshwa kwayo, pamoja na maafisa wa uhamiaji na polisi walioongozana naye, walizuiliwa Nigeria kwa karibu wiki nzima!

Uchina ilipowafukuza raia wa Nigeria, serikali ya Nigeria iliokota mamia ya raia wa Uchina waliokuwa wakifanya biashara ndogo-ndogo Nigeria ikawatafutia makosa, ikawafukuza!

Ijapokuwa Nigeria ina sera zinazoyalazimisha mataifa mengine kuiheshimu, na uchumi wake ni mkubwa zaidi Afrika, inalemazwa na ufisadi na utawala mbaya.

Ushawishi kamili wa taifa hilo utasikiwa kote duniani litakapoyathamini maadili mema. Rais atakayechaguliwa leo ana jukumu la kuongoza mabadiliko chanya nchini humo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Matiang’i apuuza mwaliko wa kuandikisha taarifa...

Ruto aendelea kufyeka watu walioteuliwa na Uhuru serikalini

T L