• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
DOUGLAS MUTUA: Mwafrika awe suluhisho la ubaguzi wa rangi duniani

DOUGLAS MUTUA: Mwafrika awe suluhisho la ubaguzi wa rangi duniani

NA DOUGLAS MUTUA

UBAGUZI uliojikita katika rangi ya watu haujawa na manufaa yoyote kote duniani, lakini mwanadamu na upumbavu wake haishi kubagua.

Hawezi kujizuia, ni kama mraibu wa dawa za kulevya.

Kwa kawaida, anayebagua ana matatizo yake mwenyewe ila akataka kujiondolea lawama kwa kuwalaumu watu wasiohusika kwa vyovyote na matatizo yake.

Japo ubaguzi humpa kuridhika kwa muda, matatizo yake hayaishii hapo, hivyo yeye hujipata katika mahangaiko ambayo hayana mwisho.

Taifa la Tunisia limejipata mashakani baada ya Rais Kais Saied kutoa matamshi ya kuwabagua watu weusi – wanaotoka kusini mwa Jangwa la Sahara – wanaoishi nchini humo.

Kutokana na madai ya kiongozi huyo kwamba ‘kuna njama ya kihalifu’ ya kubadilisha rangi ya watu wanaoishi Tunisia, watu weusi wameshambuliwa na kubaguliwa.

Sasa taifa hilo linakabiliwa na tatizo la kifedha linaloweza kumwondoa kiongozi huyo mamlakani kwa kuwa Benki ya Dunia imekataa kulikopesha pesa linazohitaji kwa dharura.

Mkutano kati ya Tunisia na Benki ya Dunia ulionuiwa kuzua mikakati ya kulinusuru kifedha taifa hilo umeahirishwa bila ya tarehe nyingine kutolewa, hivyo kuna wasiwasi tele.

Labda kisa cha Tunisia kitakuwa somo kwa mataifa mengine ya Afrika Kaskazini ambayo yamelaumiwa mara kadhaa kwa kujichukulia kama ya Kiarabu na kuwabagua watu weusi.

Tumesikia malalamiko kadhaa kutoka kwa watu weusi dhidi ya mataifa ya Tunisia, Misri, Aljeria, Libya, Morocco na mengineyo ambayo huamua kuwa sehemu ya Afrika hali inapoyafaa.

Wakati ambapo hakuna chochote cha kujivunia katika eneo la kusini mwa Sahara, mataifa hayo hujinasibisha na yale ya Kiarabu ilhali yangali wanachama wa Muungano wa Afrika na barani Afrika kijiografia.

Kumbuka maudhi ya Morocco pale timu yake ya soka ilipofanikiwa sana wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka jana na kukariri kuwa mafanikio hayo ni kwa heshima za mataifa ya Kiarabu!

Rais wa zamani wa Libya, marehemu Kanali Muammar Gaddafi, hakusita kuwakumbusha Waarabu wanaoishi Afrika kwamba wao ni Waafrika na wanapaswa kutangamana na bara lote.

Angefufuka na kupata nchi yake imegeuzwa soko la kuuzia watumwa weusi kutoka mataifa mengine ya bara hili angetamani afe tena, afukiwe kaburini mara moja.

Tusemezane ukweli: Tatizo la ubaguzi wa rangi barani Afrika si la Waarabu pekee. Watu weusi, ijapokuwa kwa mamia ya miaka wamekuwa wahanga wa tatizo hilo, pia ni wabaguzi.

Wafanyabiashara wa Kenya bado hawajaacha kuteta kuhusu duka kuu la China Square ambalo linauza bidhaa kwa bei ya kutupwa, kisa na maana linamilikiwa na Wachina.

Utamsikia mtu mzima unayetarajia atumie akili vizuri akikuuliza iwapo Mkenya anaweza kuruhusiwa kuanzisha duka kama hilo nchini Uchina!

Bila shaka wapo Wakenya wengi ambao wamepiga kambi nchini Uchina, wakiuza bidhaa na hata wakitoa huduma ya kuzisafirisha hadi mataifa zinakohitajika.

Hata hivyo, hata ingekuwa kwamba Waafrika hawaruhusiwi kufanya biashara huko, ni lazima nasi tujiunge na huo upumbavu wa kuwabagua watu?
Hatuwezi kutoa suluhisho la ubaguzi ambao umetuathiri vibaya tu tangu enzi za biashara ya utumwa? Hivi kubagua watu kwa msingi wa rangi yao hakuchoshi moyo na akili bure?

Ikiwa umekuwa mhanga wa chuki, kisha mwenyewe ukachukia watu na kuwabagua, basi unamsadikisha aliyekuchukia kutoka mwanzo kwamba ulistahili kuchukiwa.

Mwafrika anapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si tatizo, la chuki inayotokana na ubaguzi wa rangi ambayo ingali inasambaa duniani. Nao wabaguzi waadhibiwe vikali.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Msimu wa mvua nyingi kuanza – Utabiri

Ashtakiwa kwa kumchoma ‘ex’ kwa maji moto

T L