• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
DOUGLAS MUTUA: Putin ni papa nayo ICC dagaa?

DOUGLAS MUTUA: Putin ni papa nayo ICC dagaa?

NA DOUGLAS MUTUA

KUNA msemo wa Kiingereza usemao kwamba hata saa iliyoharibika huwa sahihi angaa mara mbili kwa siku.

Imedhihirika kwamba kuna ukweli fulani katika manung’uniko ya Waafrika ambao wamekuwa wakidai eti Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inawaonea viongozi wao.

Mwanzoni manung’uniko hayo yalisikika kama kelele za watu dhaifu wasiozijua haki zao, waliokuwa radhi kuwafia viongozi wanyanyasaji badala ya kuwezesha kuwaadhibu.

Ungetarajia dunia nzima ishangilie kwamba Rais wa Urusi, Vladmir Putin, ambaye anaendeleza vita nchini Ukraine, ametolewa kibali cha kukamatwa na ICC.
Mwongoza Mashtaka wa mahakama hiyo amemfungulia mashtaka pamoja na mshukiwa mwingine mmoja kwa kuwahamisha watoto wa Ukraine kwa lazima hadi Urusi.

Ajabu akidi, dunia nzima imeungana kutilia shaka uwezekano wa kibali hicho kutekelezwa, kimsingi kila mmoja akizingatia kwamba Putin ni papa mbele ya dagaa.

Hata Waafrika wanakubali kwamba huyo ni mtu mashuhuri duniani – kiongozi wa taifa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wanajiuliza atashikwaje, yaani ashuke kiwango, atoshane na watu kama Rais wa Sudan aliyepinduliwa Omar al-Bashir, Rais Mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta, Rais wa sasa wa Kenya William Ruto na wengine.

Viongozi hao, na wengine wengi wa kiwango cha chini kutoka Afrika, ama wamekuwa wageni wasio hiari au washukiwa wa ICC nyakati mbalimbali.

Wametolewa kama mifano na Waafrika wanaotaka kutusadikisha kwamba Mahakama ya ICC imejaa maonevu yaliyojikita katika ubaguzi wa rangi.

Ajabu iliyoje kwamba mtizamo huo – ambao binafsi sikubaliani nao kwa kuwa naamini kiongozi dhalimu ni zimwi likulalo likakwisha – unakubaliwa kote duniani kimoyomoyo. Utawasikia wajuzi wa sheria wakitoa visingizio vya Putin kutoweza kukamatwa, eti Urusi si mwanachama wa Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC.
Hawasemi ukweli kamili kwamba ICC yenyewe ni taasisi ya Umoja wa Mataifa, ambayo utendakazi wake unapaswa kuungwa mkono na wanachama wote.

Ukweli kwamba hiyo ni mahakama ya Waafrika na mataifa mengine hafifu usingekubalika, basi kusingekosekana shinikizo la Putin atiwe mbaroni akizuru nje!

Ziada, Putin ataponea kwa kuwa kuna mataifa yenye ushawishi – mathalan India na Uturuki – yaliyokataa kuungana na yale ya Magharibi kumkashifu kwa kuivamia Ukraine.

Ni uhalisia wa kuwavunja nyoyo watu wanaopigania usawa wa kisheria duniani, eti kibali kimetolewa kumkamata nduli hali hakuna anayeweza kuthubutu kumgusa. Hata hivyo, ninakataa kushika tama na kuhuzunika kwa kuwa ni dhahiri kwamba usawa wa kisheria ni suala la kufikirika tu, halina uhalisia wowote.

Kibali cha kumkamata Putin, japo kwa sasa hakionekani kuwa na nguvu zozote, kitakuwa na athari kubwa mno za kisiasa katika muda si mrefu ujao.

Ghafla Putin ataanza kunuka kama kicheche, yule mnyama mla kuku wa watu na mchokoaji takataka ambaye akipita karibu nawe, hata ikiwa humwoni, utajua yupo.

Kwamba akizuru taifa la kigeni atagonga vichwa vya habari kuhusiana na kibali cha kumkamata, hata ikiwa hatakuwa katika hatari ya kukamatwa, ni pigo la kisaikolojia. Wanadiplomasia wa Urusi kote duniani wataanza kuonekana kama wawakilishi wa mtoro wa kimataifa aliyezidi kwa unyama kiasi cha kuwahamisha watoto makwao!

Wanaotamani kumng’oa mamlakani wanapiga dua fursa ijitokeze; pindi atakapoisha nguvu watamvizia kama simba-marara, alivyofanyiwa Bashir wa Sudan!

Ili kuipa nguvu ICC, mataifa yenye ushawishi duniani, yakiwemo yanayomuunga mkono Putin, yanapaswa kumshawishi na kumshinikiza ajisalimishe.

Akifanya hivyo, ICC itakuwa imepata hadhi inayostahili, naye Putin atakuwa amefanya mapinduzi ya kidiplomasia dhidi ya mataifa ya magharibi yanayomsawiri kama mkaidi kichaa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Watumishi wa umma wanyimwa ladha ya TikTok

ODM yapinga kusajiliwa vyama vya majina yanayokikaribia

T L