• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
DOUGLAS MUTUA: Ruto na Raila watafute suluhisho kama Ethiopia

DOUGLAS MUTUA: Ruto na Raila watafute suluhisho kama Ethiopia

NA DOUGLAS MUTUA

WAGOMBANAO ndio wapatanao, wahenga walinena.

Hata wanasiasa wa Kenya hawataishi kukabana koo milele.

Kauli hiyo ya wahenga imethibitika nchini Ethiopia ambapo waasi wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) wamepatana na serikali kuu.

Ni hivi majuzi tu ambapo pande hizo mbili zilikazania macho na kutishiana, kila upande ukiwana kuuangamiza wa pili, kisa na maana mamlaka, kwa miaka miwili.

Kumbuka waasi hao walitishia kuvizia jiji la Addis Ababa ili kuipindua serikali ya Waziri Mkuu, Dkt Abiy Ahmed, naye akaapa kuwaangamiza hata kwa msaada wa majeshi ya Eritrea.

Chanzo cha vita hivyo kilikuwa jaribio la serikali kuu kuuondoa utawala wa Jimbo la Tigray na pahali pake kuwaweka vibaraka wa Addis Ababa kwa kisingizio TPLF walishambulia kambi za jeshi la taifa.

Wakati mmoja dunia ilipata mshtuko wa mwaka pale waasi hao walipoonyesha hadharani maelfu ya wafungwa wa kivita, wanajeshi wa Ethiopia hasa, waliotwaliwa vitani.

Serikali kuu nayo ilifunga njia zote za kufikisha misaada ya kibinadamu kwenye eneo la Tigray, maafa yakatokea, sikwambii na TPLF ikaorodheshwa kama kundi la kigaidi!

Ghafla Ethiopia iligeuka jukwaa la mzozo wa kidiplomasia ambapo serikali na waasi waliyalaumu mataifa tajiri kwa kuchochea vita vyenyewe.

Hatimaye jamii ya kimataifa iliingilia kati na kudhibiti hali, waliopigana wakatambua kwamba Ethiopia ni yao wote, wakalazimika kubadili misimamo yao kwa ajili ya amani.

Hivyo ndivyo ambavyo vita hivyo vilivyokosa mshindi. Hakuna upande utakaotanua kifua na kudai kwamba uliushinda wa pili ndipo amani ikapatikana.

Ili utulivu upatikane, ilibidi malengo ya awali ya kila upande ama yabadilishwe au yatupiliwe mbali kabisa kwa ajili ya amani.

Mathalan, safari ya TPLF ya kuelekea jijini Addis Ababa ili kumpindua Dkt Ahmed iliishia njiani.

Kiongozi huyo naye aliiondoa TPLF kwenye orodha ya makundi ya kigaidi. Si hayo tu! Aliwaruhusu waasi kuunda serikali ya mpito ya Jimbo la Tigray, akawapa watu alionuia kuangamiza majukumu ya kuongoza eneo lao.

Ajabu, kiongozi mkuu wa waasi, Bw Debretsion Gebremichael, alijiengua na kumruhusu msemaji na mshauri wake mkuu, Bw Getachew Reda, kushika usukani wa TPLF.

Hivyo ndivyo Waziri Mkuu Ahmed alivyomteua rasmi Bw Reda kuwa Rais wa Jimbo la Tigray, akisaidiwa na makamanda wawili wa waasi waliotishia hadharani kuipindua serikali kuu.

Hatua ya Bw Gebremichael kumkabidhi Bw Reda usukani wa TPLF ni ya kupongezwa kwani angenata mamlakani ateuliwe rais wa jimbo, ilivyo kawaida ya viongozi wetu.

Kunradhi, lakini nahisi kama ugomvi kati ya Rais wa Kenya, Dkt William Ruto, na kiongozi wa muungano wa Azimio, Bw Raila Odinga, umejikita katika tofauti ya umri wao.

Si siri Bw Odinga humrejelea Dkt Ruto kama ‘yule kijana’, naye Dkt Ruto humrejelea kama ‘yule mzee wa kitendawili’. Huko kubezana hakulifai kitu taifa letu.

Ningekuwa Bw Odinga, kwa kuwa tayari urais umeenda na Dkt Ruto na huenda na uzee wangu huu nisiupate kamwe, ningemteua kiongozi mchanga na niwe mshauri wake ili akabiliane na Dkt Ruto.

Huo ndio ushauri ambao viongozi wa kidini na wanadiplomasia wanaojaribu kuwapatanisha wawili hao wanapaswa kumpa kigogo huyo wa siasa za upinzani.

Yeye na vigogo wazee wa Azimio wakijiengua wote, watuachie barobaro wenye nguvu na akili, kamari nzima ya siasa itabadilika, wadau waanze kuheshimiana na kuogopana.

Hatua hiyo itaituliza nchi, iimarishe upinzani rasmi, imwajibishe Rais Ruto kuwatumikia Wakenya kwani hatakuwa na hakika ya kutawala kwa mihula miwili.

Jukumu la Dkt Ruto litakuwa kutambua na kuheshimu nafasi ya upinzani katika demokrasia yetu.

Vinginevyo, Rais Ruto atamzungusha Bw Odinga kwenye mduara usio na mwisho huku nchi ikiwa katika hali ya taharuki, uchumi ukidorora na wananchi wakiteseka.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Injera ashukuru Melrose 7s Scotland kumtambua kama shujaa

WANDERI KAMAU: Tamaa ya mwanadamu ni chanzo cha uharibifu...

T L