• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
DOUGLAS MUTUA: Suluhu ya kudumu Sudan itatoka Afrika si kwingine

DOUGLAS MUTUA: Suluhu ya kudumu Sudan itatoka Afrika si kwingine

NA DOUGLAS MUTUA

HIVI Mwafrika atawahi kufahamu kwamba yeye mwenyewe ndiye aliye na suluhu za masaibu yanayomsibu, au ataendelea kununua silaha kujiangamiza mwenyewe?

Siku chache zilizopita, anga iliponuka baruti nchini Sudan, watu wakawa wanauawa kiholela tu, mataifa tajiri yalikimbia kule na kuondoa raia wao upesi!

Mataifa hayo kwanza yaliyashawishi majeshi yanayopigana yakasitisha vita, ghafla ndege zikatua jijini Khartoum na kutekeleza shughuli hiyo muhimu.

Ijapokuwa mataifa hayo yaliwaokoa maafisa wake waliokwenda Sudan kwa shughuli rasmi, yaliwahimiza raia wayo waondoke, na kila raia aliyetaka alisaidiwa kufanya hivyo.

Shughuli ya kuwanusuru wageni hao mashuhuri ilipokamilika tu, majeshi ya taifa na kikosi maalumu kiitwacho Rapid Support Forces (RSF) yalirejelea vita, kuuana bila tafakuri.

Taarifa za maridhiano zilianza kutolewa na mataifa hayo tajiri, ila kutoka maeneo ya mbali na salama. Hata mataifa ya Afrika yalijitiatia kuwaambia ndugu wao waache kuuana.

Kimsingi, amani ya Sudan si muhimu tena kwa dunia nzima, yaani si suala la dharura, linaweza kushughulikiwa polepole. Hakuna chochote cha kuwavutia wawekezaji wa kigeni wanaotoka mataifa hayo tajiri eti kwenda kuwekeza fedha zao Sudan, hivyo maslahi ya mataifa hayo hayamo hatarini.

Kumbuka uwezekano wa Sudan kutoa mafuta ulipungua sana ilipogawanywa kukawa na Sudan Kusini kwa kuwa visima vingi vya mafuta viko eneo la kusini.

Hali ilivyo sasa ni kwamba taifa la Sudan Kusini ni kivutio kikubwa cha wawekezaji kuliko Sudan ya Khartoum. Maendeleo ya miundo-mbinu yakipatikana Sudan Kusini, wenyeji wa jangwa liitwalo Sudan wanaweza kuendelea kuota jua na kushambuliana kwa makombora ghali na hatari. Machafuko yaliyozuka Iraq, Afghanistan, Libya na kwingineko yamethibitisha kwamba, kutokana na tofauti za kiutamaduni, mataifa ya magharibi hayawezi kudhibiti nchi hizo.

Hivyo basi, hata moyo wa kujaribisha kuwashawishi Wasudan wakomeshe vita, ili miaka ya baadaye wawe washirika wa mataifa yaliyoendelea kiuchumi, haupo. Sababu kuu inayoweza kuyarejesha nchini Sudan mataifa yaliyoendelea ni hali ya vita ikiharibika sana, wahofie kwamba huenda magidi wakapata ngome mpya.

Kumbuka ugaidi hukulia katika mazingira ya machafuko na uvunjifu wa sheria, hivyo Sudan ikiendelea kuwaka kwa muda magaidi wa kigeni watafika huko na kukita kambi.

Hali nyingine inayoweza kuwashurutisha viongozi wa mataifa yaliyoendelea kuangalia Sudan kwa jicho la tatu ni hatari ya mgogoro huo kuvuka mipaka na kuingia nchi nyingine.

Hatari hizo zisipoibuka, basi wageni hao watatwaa majembe wakalime, ndugu walane maini na wakichoka waache.

Nakumbuka nikiliandikia mno suala la utengano kati ya Sudan na Sudan Kusini, nikihoji kwamba hatua hiyo haingezipa amani nchi zote mbili. Waliozoea kumwaga damu ya binadamu wenzao watatafuta sababu ya kuimwaga hata anayedhaniwa kuwa adui mkuu akiondoka, hivyo utengano haukuwa suluhu ya kudumu.

Utabiri huo umetokea kutimia kwa kuwa nchi zote mbili hizo zinakabiliwa na misukosuko ambayo mwisho wake hauonekani kuwa karibu. Ili makundi mawili yanayopigana Sudan yaridhie kuacha vita na kuishi kwa amani milele, mataifa ya Afrika yanahitajika kujituma katika kutafuta suluhisho.

  • Tags

You can share this post!

Huduma zakwama kaunti zikitatizika

NYOTA WA WIKI: Kevin de Bruyne

T L