• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
DOUGLAS MUTUA: Waafrika watafute mbinu za kusuluhisha matatizo yao

DOUGLAS MUTUA: Waafrika watafute mbinu za kusuluhisha matatizo yao

NA DOUGLAS MUTUA

HIVI Waafrika wana nia ya kusuluhisha matatizo yao kivyao, bila kuwahusisha wageni, au wao ni ‘domo-kaya’ tu?

Nimesalitika kulitafakari hili baada ya kumsikia Rais William Ruto wa Kenya akiwasuta Waafrika wanaosisitiza eti wajisuluhishie mambo ila hawawajibiki kifedha kamwe.

Dkt Ruto alilalamika hivyo akizungumza kuhusu mgogoro unaoendelea nchini Sudan, ambako majeshi yanapigania kudhibiti mamlaka.

Kando na kuwaambia majenerali wanaohusika ‘wakomeshe upuuzi huo’, alisema Waafrika hawawezi kuendelea kusisitiza kuhusu suluhu zao wenyewe ilhali juhudi zenyewe zinafadhiliwa na wageni.

Alisema vita hivyo vinafanywa na Waafrika, vinaharibu miundo-mbinu ya Afrika, pamoja na kuwaua wanawake na watoto Waafrika. Kinaya! Ukiichukulia kijuujuu tu kauli yake hiyo, utasalitika kusema kwamba Dkt Ruto ananuia kuwafurahisha wageni waliompa kazi ya kuwapatanisha majenerali hao.

Tangu hapo huwezi kuung’ata mkono unaokulisha, hivyo lazima utumie akili. Hatujui kilichomsukuma kuyasema hayo hasa.

Hata hivyo, nadhani kauli yake ina ukweli fulani. Serikali za Afrika zimegeuka omba-omba hivi kwamba tatizo likizuka popote katika bara hili, mataifa wanachama wa Muungano wa Afrika (AU) hujikokota kulitatua.

Waafrika wanatarajia mataifa tajiri kama Marekani, Ujerumani, Uingereza Ufaransa, Japan, Uchina, Urusi na kadhalika kutoa pesa, wao waalikwe kuhudhuria vikao tu. Na ikitokea kwamba vikao vile havina posho, basi hakuna anayetaka kushiriki! Anachokitaka Mwafrika ni pesa za bwerere, apokee wala asitoe, zisipotoka humwoni pale! Hizo ni fikra za aina gani kwa mtu anayedai kutaka kujitawala?

Tangu hapo anayekulisha anakudhibiti; ukijulikana wewe mlafi, tumbo lako litashughulikiwa upesi, wanaokijua kinachotakiwa kufanywa ili kujinufaisha waingie kazini kupanga mikakati ya kukurithi huku ukila na kucheua.

Nimeandika hapa awali kuwa mgogoro wa Sudan unahitaji kushughulikiwa na Waafrika wenyewe, na kufanya hivyo si kuhudhuria vikao na kupata posho za wafadhili tu.

Ni sharti Waafrika wagharimike, wawe na mfumo wa kushughulikia mizozo ya kisiasa na majanga ya kiasili yanayoweza kulikumba bara hili kama vile dhoruba, mafuriko, maporomoko ya ardhi na hata mlipuko wa maradhi.

Ni kutokana na tabia yao ya kuombaomba ambapo kote duniani viongozi wa Afrika huonekana kama kupe au watu wajanja wasiotaka kujituma katika kubadilisha hali yetu.

  • Tags

You can share this post!

Rai Serikali ihifadhi vyumba vya mateso Nyayo kama...

TAHARIRI: FKF ichunguze malalamiko yanayoibuliwa kuhusu...

T L