• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
DOUGLAS MUTUA: Wakenya waliofungwa jela Uganda hawafai kuokolewa

DOUGLAS MUTUA: Wakenya waliofungwa jela Uganda hawafai kuokolewa

NA DOUGLAS MUTUA

UGANDA inastahili pongezi kwa kutuonyesha jinsi ya kukabiliana na wahalifu waitwao wezi wa mifugo; imewafunga Wakenya 32 kifungo cha miaka 20!

Kilichonipendeza zaidi si kifungo hicho tu bali pia sheria iliyotumika kuwatia adabu waja hao ambao wametusumbua kwa miaka mingi.

Nchini Uganda ipo sheria inayosema kwa kuwa silaha ni milki ya vikosi vya ulinzi na usalama pekee, yeyote anayezimiliki kinyume na sheria atashtakiwa na kuhukumiwa katika mahakama ya kijeshi.

Hiyo ndiyo sheria tunayohitaji nchini Kenya, lakini kwa kuwa kila kitu nchini mwetu kinatiwa siasa, ukabila na visingizio vinginevyo, ni vugumu kwetu kuipitisha. Tukijaribu kutunga sheria kama hiyo, watu fulani watadai wizi wa mifugo, katika karne hii, ni utamaduni wao.

Binafsi ningewaelewa kikamilifu wizi huo ungekuwa maigizo tu, kwa mfano kuwe na mpango mifugo ‘ikiibwa’ irejeshwe kirafiki bila umwagikaji wa damu.

Lakini uhalisia ni kwamba wizi wa mifugo si mchezo, ni uhalifu hasa, ambapo watu wengi huuawa na kusahaulika kana kwamba maisha yao hayana thamani.

Serikali ya Nairobi – kama inavyoitwa na watu waishio mbali nayo – huruka juu na kuteta tu ikitokea kwamba afisa wa polisi au mtu mashuhuri ameathirika.

Tumetokea kuwathamini watu wa mijini hivi kwamba mmoja pekee akiuawa, kwa mfano, mjini Thika, habari zake zitachapishwa magazetini hadi atakapozikwa. Ngoja wanawake na watoto wauawe kwa makumi kaskazini mwa nchi na wahalifu hao, watapuuziliwa mbali kuwa ni wahanga wa wizi wa mifugo. Hautupigi mshipa!

Kila maisha yana thamani, na Kenya ni yetu sote, hivyo serikali pamoja nasi watu binafsi hatupaswi kukubali kwamba ni kawaida kwa baadhi yetu kuuawa kikondoo. Kwamba shughuli ya kuwasaka wezi wa mifugo iliyoanzishwa na serikali ya Kenya majuma kadha yaliyopita ikihusisha vikosi mbalimbali vya usalama haijazaa matunda ya kusifiwa ni aibu kuu.

Nchini Uganda, serikali imesikia tu kuwa kuna silaha zilizofichwa zizini kwenye mpaka wake wa kaskazini, ikawatuma maafisa wake huko, habari ikaibukia mahakamani watu wakikiri makosa yao! Mbona kwetu hali ni tofauti?

Namkumbuka Gavana wa sasa wa Trans Nzoia, Bw George Natembeya, akihadithia jinsi shughuli za kuwasaka wahalifu hao zilivyokuwa zikivurugwa na watu mashuhuri serikalini enzi akiwa Kamishna wa eneo la Bonde la Ufa.

Alifichua kwamba kila wakati vikosi vilipoambiwa wahalifu wamejificha eneo fulani, viliangusha mabomu eneo tofauti kwa makusudi. Kisa na maana? Kwenye ile meza ya kupanga mikakati ya kukabiliana na wahalifu hao, walikuwepo watu waliofaidika na wizi wenyewe! Hawangejihini.

Imekuwaje kwamba nchi yetu ina watu wanaoitwa ‘mashuhuri’, ila wako radhi kuendesha uhalifu unaoishia kwa vifo vya watu, huku wakiwalinda wahalifu kwa ajili ya maslahi yao?

Sheria kama hiyo ya Uganda ikitumika nchini Kenya, watu hao mashuhuri watatafuta wezi wa kutumia wawakose kwa kuwa kila mmoja ataogopa kuozea gerezani.

Hata wahalifu wanaotishia watu na kuwaibia magari kwa bunduki mijini wataogopa kwa kuwa tangu hapo tukiamini majeshi hayacheki na mtu.

Hata hivyo, sheria yenyewe itatumika vizuri ikiwa washukiwa watalindiwa haki zao.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: FKF iingilie mzozo kati ya makocha Aussems, Matano

WANDERI KAMAU: Hatua zichukuliwe kuwaokoa Wakenya...

T L