• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
TAHARIRI: GMO: Serikali ielimishe wananchi kuondoa dukuduku

TAHARIRI: GMO: Serikali ielimishe wananchi kuondoa dukuduku

NA MHARIRI

HATUA ya serikali kuondoa marufuku dhidi ya mahindi ya GMO imezua mjadala mkali nchini.

Suala la GMO limetekwa nyara na wanasiasa huku mamilioni ya Wakenya wakijipata njia panda bila kujua ukweli kuhusu mahindi hayo.

Viongozi kutoka maeneo yanayokuza mahindi, kwa mfano, wamejitokeza kupinga mpango wa serikaliw kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi ya GMO.

Viongozi hao – wengi wao wakiwa wandani wa Rais William Ruto – wanataka mahindi hayo ya GMO yaletwe baada ya wakulima kuuza mahindi wanayovuna sasa.

Baadhi ya wanasiasa wametishia kumtimua waziri wa Biashara Moses Kuria kwa kuagiza mamilioni ya magunia kutoka ng’ambo ilhali wakulima wamekwama nyumbani na mamilioni ya magunia ya mahindi.

Bila shaka, kupinga huko kunatokana na hofu kwamba huenda wakapoteza kura katika uchaguzi wa 2027 iwapo mahindi ya GMO yatasababishia wakulima hasara kubwa ilhali wao wamesalia kimya.

Ikiwa kweli viongozi hao kutoka muungano wa Kenya Kwanza wanapinga mahindi ya GMO, mbona wanakimbilia kuhutubia wanahabari badala ya kukutana na Rais Ruto kumwelezea malalamishi yao?

Kundi jingine la wanasiasa likiongozwa na kinara wa Azimio Raila Odinga linapinga kwa kigezo kwamba serikali haikushauriana na wananchi kabla ya kuondoa marufuku dhidi ya mahindi ya GMO.

Bw Odinga na kundi lake pia anadai kuwa mahindi hayo yanasababisha kansa kati ya maradhi mengineyo.

Kinaya ni kuwa Bw Odinga alipokuwa waziri mkuu alikuwa miongoni mwa watetezi wakuu wa mahindi ya GMO kabla ya kupigwa marufuku mnamo 2012.

Juzi Bw Odinga alisema kwamba alilazimika kubadili msimamo wake baada ya kupata ushahidi uliomfanya kuridhika kwamba mahindi ya GMO ni hatari kwa afya.

Nao viongozi wa kidini, wamejitokeza kushutumu vikali matamshi yaliyotolewa na Waziri Kuria kuhusiana na GMO lakini hawasemi ikiwa wanapinga au kukubali mahindi hayo.

Kwa upande wake, serikali haijaonekana kuweka bidii katika kuelimisha wananchi kuhusu faida au madhara ya mahindi ya GMO.

Serikali imeshikilia kwamba inataka kuleta magunia milioni 10 ya mahindi GMO kuokoa karibu Wakenya milioni 4.5 wanaokabiliwa na makali ya njaa.

Viongozi wakuu serikalini ambao wamejitokeza kuzungumzia GMO wanatoa matamshi ya kuogofya zaidi wananchi badala ya kuwapa matumaini.

Kwa mfano, Waziri Kuria amekuwa akitoa kauli za kuogofya kwa kusema kuwa ‘watu watakufa tu hata bila kula mahindi ya GMO’.

Kauli hiyo inaweza kufasiriwa kuwa serikali haijali afya ya raia wake.

Ukweli ni kwamba, mbali na utafiti tatanishi uliofanywa nchini Ufaransa na kudai kuwa mahindi ya GMO yanasababisha kansa, hakuna utafiti mwingine ambao umewahi kuthibitisha madai hayo.

Serikali iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata taarifa sahihi kuhusu GMO badala ya kuachia wanasiasa kujibizana huku wakitoa madai ya kukanganya wananchi.

You can share this post!

Kenya Kwanza yaanza kutikiswa na mivutano

CHARLES WASONGA: Ruto azingatie ahadi yake ya kutoangusha...

T L