• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
JUMA NAMLOLA: Ni kazi bure kuahidi kuimarisha uchumi bila kudhibiti ufisadi

JUMA NAMLOLA: Ni kazi bure kuahidi kuimarisha uchumi bila kudhibiti ufisadi

NA JUMA NAMLOLA

WIKI hii hapa katika meza ya habari ya Taifa Leo tuliangazia mambo ambayo wanasiasa wote waliojitokeza kutamani uraia mwaka ujao, wamekataa kuyaangazia.

Kubwa zaidi kati ya mambo hayo ni hili donda ndugu la ufisadi. Kitendo hiki kinato – kana na neno la Kiarabu ‘Fasad’ lenye maana ya uozo, uharibifu na uenezaji wa maangamizi katika ardhi. Pia Fasad ni kuenda kinyume na kanuni alizoweka Mungu.

Hebu chukua mfano kwamba mwanafunzi katika chuo cha udaktari hahudhurii masomo. Kwa kuwa familia yake ina pesa, anamhonga mhadhiri ampitishe kwenye mtihani.

Mtu huyo anapofuzu udaktari, kweli wagonjwa watakuwa salama? Au mtu ambaye hakushika masomo kuhusu uendeshaji ndege. Je, akitoa hongo na kufuzu urubani, utakuwa tayari kupanda ndege anayoiendesha?

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amekaribia suala la ufisadi kwa kutangaza kuwa atawafunga wafisadi. Hajaeleza atawafunga vipi, ikizingatiwa kuwa yeye iwapo atachaguliwa, atakuwa rais na wala si jaji katika mahakama.

Naye Dkt William Ruto sijamsikia akisema chochote kuhusu mbinu alizo nazo kumaliza ufisadi. Kama amewahi kusema hili, naomba nifahamishwe.

Ufisadi ndilo tatizo la kushughulikiwa kwa dharua. Hata sasa! Hatutasubiri hadi Agosti au Oktoba mwaka ujao kuanza kukabili jinamizi linalomnyima mlipa ushuru thamani ya pesa zake.

Ni wiki hii tu ambapo wizara ya Afya iliwatisha raia kwa kuwaambia, wasipochanjwa kufikia Disemba 21, watakatazwa huduma muhimu.

Nasema ni kuwatisha kwa sababu serikali ina njia nyingi za kutumia na kushawishi watu wafanye jambo. Lakini waziri wa Afya Mutahi Kagwe alipotoa tangazo hilo, ni kama hakuwa amefanya utafiti wake ipaswavyo.

Sasa imebainika kuwa, baadhi ya maafisa katika wizara ya Afya wanauza vyeti vya kuonyesha watu wamechanjwa dhidi ya virusi vya corona.

Uhuni huu utatuharibia sifa kama taifa, na kusababisha waliochanjwa kilalali wakataliwe na taasisi za kimataifa.

Mwandishi ni mhariri wa habari katika gazeti la Taifa Leo [email protected]

 

You can share this post!

PETER NGARE: Tusihadaike eti ‘kazi ni kazi’ wala pesa...

FC Talanta yapata matokeo mseto kocha akilalama

T L