• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
JURGEN NAMBEKA: Kaunti nyingine Pwani ziige ‘Mombasa Yangu’ ya Nassir

JURGEN NAMBEKA: Kaunti nyingine Pwani ziige ‘Mombasa Yangu’ ya Nassir

NA JURGEN NAMBEKA

MAJUZI Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswammad Nassir, alianzisha mpango wa ‘Mombasa Yangu’ unaonuia kutoa nafasi za ajira kwa vijana 2,000.

Tayari vijana kadhaa katika kaunti hiyo wamepewa ajira, na kupunguza, japo padogo, idadi ya wasio na kazi.

Manufaa yake pia yameanza kuonekana jijini Mombasa kwani mandhari yake yamekuwa safi zaidi; vijana hurauka kila siku kulisafisha hasa eneo la katikati.

Vijana mbalimbali pia wamepokea mafunzo ya kujiendeleza katika sekta za utoaji huduma kama vile wahudumu wa kukabiliana na mikasa, na askari wa kaunti.

Mpango huu unashika kasi na unawapa changamoto magavana wa kaunti tano zingine za Pwani kusaka njia za kukabiliana na jinamizi la ukosefu wa ajira.

Ukosefu wa ajira Pwani umesukuma vijana wengi katika uraibu wa dawa za kulevya na hivyo kukosa mwelekeo maishani.

Hatua aliyochukua Gavana Nassir iliungwa mkono na Rais William Ruto, ambaye aliahidi kuongeza vijana wengine 2,000 kwa ajili ya upanzi wa miti na utunzi wa mazingira.

Bw Nassir amewapa changamoto magavana wa Kwale, Tana River, Kilifi, Lamu na Taita Taveta kukuna vichwa zaidi ili kuhakikisha vijana wote wanapata ajira.

Japo mpango huo ni mdogo kwa sasa, ukipigwa jeki utachangia pakubwa kuzima jinamizi la ukosefu wa ajira Pwani na taifa kwa jumla, ili miaka ijayo liwe limezikwa katika kaburi la sahau.

Katika Kaunti ya Kwale Bi Fatuma Achani anaweza kuanzisha mradi kama huo kusaidia vijana kuweka akiba ambayo baadaye wanaweza kuanza miradi yao.

Kupitia mpango huo, magenge ya vijana yanayowakaba koo wakazi na kuwaibia kimabavu, hakika yatapungua.

Kwa kujua kuna njia halali na safi ya kujipatia kipato, wengi wataacha mienendo isiyofaa na kuzamia ajira watakazopewa.

Aidha Lamu, Malindi, Watamu na Diani ni miji ya kitalii sawa tu na Mombasa.

Magavana wa miji hiyo wakitenga kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya mpango sawa na huo, kutaongeza juhudi za miji yao kuwa safi.

Isitoshe, vijana wanapojiunga na idara kama ile ya wazimamoto wa kaunti, basi nguvukazi zaidi zitakuwepo kutekeleza kazi zinazolemea wahudumu wakongwe.

Kwa vijana kujifunza kazi hizo za kiufundi ama zile zinazohitaji ujuzi zaidi, wataweza kukua kitaaluma na kutoa huduma bora kwa wakazi.

Wazo la Gavana Nassir ni la kuigwa. Itakuwa vyema kaunti zingine Pwani zikifuata mkondo uo huo, kwani yote ni kwa ajili ya kufanikisha maisha ya usoni ya vijana wao na mwishowe taifa kwa jumla.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaahidi kuwasaidia wakulima kuimarisha uzalishaji...

KINYUA KING’ORI: Tujadili mbinu za kukabili...

T L