• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
JURGEN NAMBEKA: Kaunti zisiwafedheheshe wazazi wanaosaka basari

JURGEN NAMBEKA: Kaunti zisiwafedheheshe wazazi wanaosaka basari

NA JURGEN NAMBEKA

WAZAZI katika kanda ya Pwani wamelalamikia jinsi shughuli ya kutolewa kwa basari za kufadhili masomo ya wanawao inaendeshwa katika kaunti kadhaa.

Katika Kaunti ya Kilifi, idadi kubwa ya wanafunzi walikuwa hawajaripoti shuleni kwa kukosa karo na pesa za matumizi shuleni.

Gavana Gideon Mung’aro alikuwa ameeleza wazazi kwamba wanafunzi wao wangepata tu basari baada ya kujiunga na shule walizoitwa kwanza.

Kule Mombasa, wazazi wenye ghadhabu walijitokeza kuchukua fomu za basari huku wakilalamikia jinsi walivyohudumiwa.

Mmoja wao aliteta kuondolewa kwa foleni na kutakiwa kwenda shule kumchukua mwanawe kisha aje apige mstari huo.

Cha kuvunja moyo ni kuwa fomu si hakikisho la kupewa basari kwani baada ya kuzijaza lazima mwanafunzi apitie mchujo kabla kupata usaidizi huo.

Kwa ujumla, takriban wanafunzi 2,000 Pwani walikuwa wameshindwa kujiunga na shule za upili kwa kukosa fedha.
Inahuzunisha kwani hawa viongozi wa kesho wanakosa elimu.

Bw Mung’aro wiki iliyopita alidokeza kuwa idadi ya wanafunzi waliohitaji msaada wa masomo ilikuwa imeongezeka na kulikuwa na haja ya kuongeza fedha za basari kutoka Sh350 milioni hadi Sh1 bilioni.

Je, kaunti za Pwani zaweza kujiandaa vipi kwa shughuli hiyo?

Kwanza, wazo la serikali za kaunti kuongeza mgao wa fedha za ufadhili litasaidia sana kukabiliana na tatizo hilo.
Huenda pia serikali hizo zikatenga hela spesheli kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga na shule za upili, ili masomo yao yasitatizike haswa iwapo wamefanya vyema katika mitihani yao.

Pili, serikali za kaunti zinaweza kushirikisha sekta ya kibinafsi, kama inavyofanya katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kutafuta wahisani na wafadhili wa kuwekeza katika elimu ya wanafunzi kutalegeza mzigo huo mzito kwa wazazi wasiojiweza.
Aidha, serikali inaweza kusaini mikataba na shule za kibinafsi kutoa ufadhili wa masomo kwa angalau wanafunzi wawili, ili kusaidia watoto maskini.

Kaunti ziendelee kuhamasisha jamii umuhimu wa masomo ya wanafunzi, na hata kurai wanajamii walio na uwezo kutoa msaada kwa wanafunzi maskini.

Inasikitisha sana kuona wanafunzi waliojitolea kutia bidii masomoni, wanasalia nyumbani kisa ni ukosefu wa karo.

Ni ombi langu kuwa serikali ya kitaifa na za kaunti zitasaka njia mwafaka kuhakikisha wanafunzi wote waliofanya mtihani wanajiunga na shule za sekondari.

Inahuzunisha kwa wazazi wao kufedheheshwa wanapotia jitihada kutafuta basari ili wanafunzi hao wapate elimu ya upili.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wabunge wa kike waangazie shida za jamii zilizo...

Romelu Lukaku abeba Inter Milan dhidi ya FC Porto katika...

T L