• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 1:47 PM
JURGEN NAMBEKA: Magavana waipe kipaumbele miradi muhimu iliyokwama

JURGEN NAMBEKA: Magavana waipe kipaumbele miradi muhimu iliyokwama

NA JURGEN NAMBEKA

WAKAZI wa kisiwa cha Dongo Kundu katika Kaunti ya Kilifi hivi majuzi walijitokeza kulalamikia kutokamilishwa kwa daraja la urefu wa kilomita moja, ambalo litawasaidia kuingia na kutoka kisiwani.

Mradi huo ulilenga kuwaondolea masaibu ya kupitia baharini na kisha katika kijia cha pekee cha kuingia katika kisiwa hicho.

Isitoshe, daraja hilo lilikuwa liwasaidie pakubwa wanafunzi wanaosoma shule zilizo nje ya kisiwa, ili wasipatwe na matatizo wakati wa kuvuka.

Licha ya maono hayo mazuri, kutokamilika kwa mradi huo kumekera wananchi na sasa wanaitaka serikali ya kaunti kuukamilisha au kuuondoa.

Wakazi walikuwa wamelazimika kuinama na kuinuka kila baada ya hatua chache, katika kijia cha pekee cha kuingia kisiwani.

Wazazi wa wanafunzi wadogo wanaosomea shule ya msingi ya Dongo Kundu, nao wamekuwa wakilazimika kuwabeba mgongoni wakiwapeleka shuleni.

Wanalalamikia kuinama huko kwenye kijia hicho, kwamba kumewaleta taabu chungu nzima.

Swali ni je, mbona serikali iache wananchi wakiteseka ilhali pesa zilishatengewa utekelezaji wa mradi huo?

Maelezo ya kauntikwamba pesa hizo zilibadilishwa mkondo kwa ajili ya miradi mingine baada ya serikali mpya kuingia mamlakani, ni hujuma kwa wakazi.

Je, inamaanisha wakazi hawapaswi kuendelea na maisha yao kwa kuwa serikali imebadilishwa?

Imebainika kuwa mradi ulitengewa fedha za kutosha, ila wanakandarasi fulani wakalipwa na baadaye wakakosa kutoa huduma zao kikamilifu.

Haileweki kwanini mradi ambao haungegharimu kaunti hiyo pesa nyingi, ukwame na kuwaacha wananchi wakitaabika.

Kwa mkazi wa kisiwa hicho, ni wazi kuwa serikali waliyoipigia kura kutwaa uongozi haiwajali.

Imewaacha kuhangaika wakifanya miinamo na mminuko ili kuingia na kutoka eneo hilo.

Inavunja moyo kwamba wakazi walirauka mapema kupiga kura na bado wanataabika kutekelezwa maendeleo yaliyo haki yao.

Mradi huu ni moja tu kati ya mingi eneo la Pwani ambayo imekwama baada ya uongozi wa serikali za kaunti kubadilishwa.

Furaha ya wakazi walioshangilia na kupiga makofi siku ya uzinduzi wa miradi hiyo, imesalia kero wanapotazama wasijue la kufanya kwa miradi kukosa kukamilika.

Ni ombi langu kuwa magavana wote wa Pwani na nchi nzima kwa ujumla, wataangalia miradi muhimu iliyokwama kutoka kwa watangulizi wao.

Kisha ipige msasa wanakandarasi waliopewa zabuni hizo na kujua mbona hawakuikamilisha, na kwamba wanawajibika ipasavyo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Matamshi ya Msimamizi wa Bajeti hayakufaa

KINYUA KING’ORI: Ufisadi: Gachagua afanye kweli na...

T L