• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
JURGEN NAMBEKA: Serikali iongeze jitihada kuzima mizozo ya watu na wanyamapori Tsavo

JURGEN NAMBEKA: Serikali iongeze jitihada kuzima mizozo ya watu na wanyamapori Tsavo

NA JURGEN NAMBEKA

KWA muda mrefu Wakenya wanaoishi karibu na mbuga za wanyamapori zilizoko Pwani, wamelalamikia uvamizi wa wanyama hao nyumbani mwao.

Uvamizi huu mara nyingi umeishia kutonesha hata zaidi mizozo kati ya wanyama wa porini na wanadamu.

Wanyama hao hutoka mbugani na kuingia katika mashamba ya wakazi kusaka lishe.

Matokeo yake ni wao kuharibu mimea na kusababishia wakulima hasara tupu.

Visa hivi vya uvamizi vimeongezeka mno hususan kwa watu wanaoishi karibu na mbuga ya Tsavo katika kaunti za Taita Taveta na Kwale.

Hii ni baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kusababisha ukosefu wa mvua, hali ambayo ilikausha visima vya maji ndani ya mbuga na kunyauka kwa majani ya lishe.

Japo wanyamapori ni fahari ya nchi kwani ni kitega uchumi kupitia utalii, mambo hugeuka wakulima wenye gadhabu wanapokumbana nao.

Katika eneo la Matuga na Shimba Hills, kwa mfano, wakulima hukesha usiku mzima kuwazuia ndovu wasivamie mashamba yao.

Hali hii ni hatari kwani wakati mwingine wanalazimika kuua ndovu hao wavamizi ama wao wenyewe kujeruhiwa vibaya na wanyama hao.

Majeraha wanayopata ni kando na mimea wanayopoteza – ambayo yangewapa mapato – na mali za kibinafsi kama nyumba.

Serikali inapaswa kuvalia njuga suala hili kwa kuhakikisha wakazi wanaoishi karibu na mbuga wanawekwa kipaumbele katika mikakati yoyote itakayobuniwa.

Kwanza, inapaswa kuunda sera maalum ya kulinda mimea ya wakulima, kwa kuwa na mpango wa kuwafidia endapo wanyamapori watavamia ardhi zao.

Pili, serikali iendeleze mpango wa kujenga nyua za umeme katika kila mbuga nchini kuhakikisha wanyama hao hawatoki katika makazi yao hayo maalum.

Tatu, iwapo wanyama hao watatoka mbugani, serikali ifadhili wakulima kujenga maghala yaliyo chini ya ardhi au yaliyoinuliwa juu kabisa ili kuzuia wanyamapori kufikia mazao yaliyohifadhiwa humo.

Nne, serikali ya kitaifa na za kaunti zianzishe miradi inayohusisha jamii katika utunzi wa wanyamapori, ili kuzuia visa vya wakulima kuua wanyamapori.

Kwa hamasisho hilo, watawafukuza tu bila kuwaumiza.

Tano, serikali italazimika kutafuta mbinu mbadala ya kuhakikisha visima vya maji ndani ya mbuga havikauki , ili kupunguza visa vya wanyama hao kuondoka mbugani kwenda kusaka bidhaa hiyo muhimu.

Yote tisa, serikali ya kitaifa na kaunti zijikune kichwa kusaka mbinu anuwai za kuzima mizozo baina ya wanyama na wakazi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Idara za serikali ziwe zinatenga malipo kabla ya...

Biden asema nchi yake imepiga hatua kiuchumi

T L