• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
JURGEN NAMBEKA: Vijana wa Pwani wajifunze kuhusu utaalamu wa gesi

JURGEN NAMBEKA: Vijana wa Pwani wajifunze kuhusu utaalamu wa gesi

NA JURGEN NAMBEKA

RAIS William Ruto alizuru Pwani kuzindua ujenzi wa kiwanda cha gesi aina ya LPG katika eneo la Dongo Kundu.

Wakati wa hafla hiyo, Dkt Ruto na viongozi wengine walimtaka Rostam Aziz kutoka Tanzania awape kipaumbele Wapwani katika ajira zitakazoibuka.

Naibu Rais Rigathi Gachagua hususan alimtaka Bw Aziz kuja na wafanyakazi wachache kabisa, yaani wawe ni wasimamizi wakuu pekee yake.

Kulingana naye Pwani ina wafanyakazi wenye tajriba ya kutosha kuendesha shughuli katika kiwanda hicho cha gesi, ila hii sio kweli.

Ni kweli kuwa sehemu kubwa ya Wapwani wanaoishi Dongo Kundu hawana ajira.

Ila swala ibuka ni iwapo wana tajriba katika sekta hiyo ya gesi; ama pengine kazi wanazotarajia ni za sulubu kama kubeba mizigo isiyohitaji tajriba.

Katika hali iyo hiyo, je kuna wahandisi waliohitimu kutoka Pwani wenye ujuzi na tajriba ya kutwaa nafasi zitakazoibuka?
Je, kuna vijana wajuzi wa masuala ya gesi na uendeshaji wa kiwanda kama hicho?

Kwa mujibu wa wakuu wa kiwanda hicho kitakachomilikiwa na kampuni ya Taifa Gas, huenda ikachukua miezi 12 kukamilika.

Hivyo, kuna mwanya wa vijana wenye uwezo na ari kuanza kujiweka katika hali nzuri kimasomo kuelewa kazi ya kiwanda hicho.

Bila kutilia mkazo hilo, malalamishi ya viongozi kuwa wananchi wa Tanzania wamesafirishwa kuja kusimamia kampuni hiyo, yatakuwepo ifikapo mwaka ujao.

Kaunti za Pwani zifanye nini kuhakikisha vijana wao ndio wanafaidika na ajira hizo, na sio tu kazi za kulima, kuchimba mitaro na kubeba mizigo?

Viongozi wa gazuti za Kwale na Mombasa, na Pwani kwa ujumla, wachukue nafasi ya kuzungumza na Bw Aziz kufahamu mafunzo yanayohitajika ili kuendesha kazi za kitaalamu katika kiwanda hicho.

Kwa kutenga pesa kiasi katika bajeti zao, kaunti hizo ziwatafute vijana wakasomee masuala ya uundaji gesi na usimamizi wa kiwanda husika.

Aidha iwapo kuna Wapwani waliohamia mjini Nairobi na hawana kazi, ila wamefuzu katika taaluma hiyo, wajiwasilishe na kutuma maombi yao mapema.

Iwapo haya hayatatekelezwa, Wapwani watapata ajira zile za kawaida tu, huku watu wengine wakitolewa mbali kuja kushughulikia uendeshaji wa kampuni hiyo.

Ni ombi langu kwamba Bw Aziz anapowekeza Sh16 bilioni katika mradi huo, Wapwani na serikali za kaunti za eneo hilo watafanya hima kuwaandaa vijana wao kwa kazi hizo.

Wasipofanya hivyo watajilaumu wenyewe kwani miezi 12 ni mingi kusoma na kufuzu.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali yafaa imalize wizi wa chakula cha msaada

UJASIRIAMALI: Ana magari ya wateja kulipia wayatumie kwa...

T L