• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
CECIL ODONGO: Mbona KKA wana kiwewe sava ya IEBC kufunguliwa?

CECIL ODONGO: Mbona KKA wana kiwewe sava ya IEBC kufunguliwa?

NA CECIL ODONGO

NAIBU Rais Rigathi Gachagua atathmini kauli zake kwani zinamsawiri kama anayepinga maridhiano kati ya Rais William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga.

Kauli za Bw Gachagua zimekuwa zikimlenga zaidi Bw Odinga kibinafsi, na huenda zikatatiza mazungumzo ambayo yamekumbatiwa kusitisha maasi nchini.

Ni Rais Ruto alianzisha nia ya kumshawishi Bw Odinga akomeshe maandamano ili kupisha mazungumzo ambapo masuala aliyoibua yashughulikiwe ndani ya Bunge. Hivyo, ni Rais mwenyewe anastahili kuzungumza au kutoa kauli kuhusu gumzo hilo.

Aidha, sharti la Bw Gachagua kwamba Raila anastahili kutambua urais wa Ruto kabla mazungumzo yaanze, halina mashiko. Hii ni kwa sababu kiongozi huyo wa muungano wa upinzani, Azimio, amekariri mara kadhaa kwamba anaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Upeo uliohalalisha ushindi wa Dkt Ruto ila hakubaliani nao.

Iwapo Bw Gachagua anataka Bw Odinga atambue ushindi wa Ruto basi nao muungano tawala, Kenya Kwanza (KKA) unastahili kuwa radhi kuruhusu mitambo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ifunguliwe ndipo ukweli ufahamike kuhusu uchaguzi mkuu uliopita.

Bw Odinga amenukuliwa mara kadhaa akisema kwamba ana taarifa za mfichuzi ndani ya IEBC kuwa alishinda uchaguzi wa urais kwa kura milioni 8.1 huku Ruto akipata milioni 5.9 pekee.

Kiini cha matatizo ya sasa nchini ni mikwaruzano kati ya upinzani na serikali kuhusu nani mshindi wa kura ya urais iliyopita. Iwapo sava ya IEBC itafunguliwa, itabainika nani ni msema ukweli kati ya upinzani na serikali.

Hivyo, Bw Gachagua anapotoa masharti kwa Bw Odinga kuwa lazima atambue ushindi wa Rais, pia atumie juhudi na nguvu zizo hizo kuhakikisha sava ya IEBC iko wazi. Ni haki ya kigogo wa upinzani kuamua iwapo atatambua urais wa Ruto au la; wala sioni kinachomwasha Bw Gachagua sababu kwa njia moja au nyingine hataondoa KKA uongozini.

Aidha, Naibu Rais pia akumbuke si mara ya kwanza matokeo ya urais nchini yanapingwa. Baada ya uchaguzi wa 1992 – wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi – upinzani ukiongozwa na Kenneth Matiba, Mwai Kibaki na Oginga Odinga, walipinga ushindi wa Rais Daniel Arap Moi.

Vivyo hivyo, Mwai Kibaki alipinga matokeo ya uchaguzi wa 1997, Raila akapinga ushindi wa Kibaki mwaka 2007, kisha Uhuru Kenyatta 2013 na 2017. Katika matukio haya yote, utawala ambao ulikuwa mamlakani haukuondolewa.

  • Tags

You can share this post!

Wezi wavamia hospitali na kupora wagonjwa

Kukosa usingizi wa kutosha kunaleta madhara haya

T L