• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
TAHARIRI: Bajeti za kaunti zizingatie pia maoni ya umma

TAHARIRI: Bajeti za kaunti zizingatie pia maoni ya umma

NA MHARIRI

RIPOTI ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali inayoonyesha kuwa mabunge ya kaunti yanapitisha bajeti kiholela bila kuhusisha wananchi, haifai kupuuzwa.

Kwa mujibu wa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu, kaunti hazikuhusisha raia katika utayarishaji wa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2021/2022. Ripoti inasema kuwa bajeti za kaunti zote 18 zilizochunguzwa zilipitisha matumizi ya fedha kutekeleza miradi isiyokuwa na umuhimu kwa raia.

Kaunti chache zilizodai kushirikisha umma katika mchakato wa utayarishaji wa bajeti, hazikutoa maelezo kuhusu mahala pa mkutano na siku za mikutano hiyo kwa wakati kuwezesha wakazi kujitokeza kutoa maoni.

Kutohusisha umma katika utayarishaji wa bajeti kunamaanisha kuwa miradi mingi inayotengewa fedha hazilengi kuwafaa raia bali kuwanufaisha wanasiasa wachache.

Huku wanasiasa wanamezea mate miradi inayowawezesha kupata kandarasi za mamilioni ya fedha, wananchi wanahitaji miradi inayowapunguzia mahangaiko kama vile maji, masoko kati ya mingineyo. Mahitaji ya wananchi katika wadi moja yanaweza kuwa tofauti na yale ya wakazi wa wadi jirani.

Kutenga raia katika mchakato wa kuandaa bajeti ni kusaliti Katiba iliyobuni mfumo wa ugatuzi. Lengo la mfumo wa ugatuzi ni kustawisha maeneo yote nchini kuanzia vijijini.

Ustawi huo hauwezi kupatikana bila kuhusisha raia ambao ni walengwa wa maendeleo hayo.

Aidha, Katiba inahitaji wananchi washirikishwe katika maamuzi yote muhimu yanayowahusu. Upitishwaji wa bajeti bila kujumuisha maoni ya wakazi unaonekana kuchangia katika ongezeko la utekelezwaji wa miradi isiyohitajika.

Mathalan, ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali iliyotolewa Machi, mwaka huu, ilibaini kuwa miradi ya jumla ya Sh55 milioni imekwama katika Kaunti ya Makueni.

Bi Gathungu alishangaa ni kwa nini miradi hiyo haijazinduliwa itumiwe na wananchi licha ya kukamilika zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Madiwani na hata wabunge wa Bunge la Kitaifa wamekuwa wakijitetea kuwa hata wakiita mikutano ya kujadili bajeti wananchi hawajitokezi.

Miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha raia kutojitokeza katika mikutano ya umma kutoa maoni ni kuwa mapendekezo yao huwa yanapuuzwa na hayajumuishwi kwenye maamuzi ya mwisho yanayofanywa na wanasiasa.

Kuna haja gani kutoa maoni yanayotupwa katika jalala la takataka na wanasiasa?

Kuna haja kwa Bunge kuharakisha upitishwaji wa Mswada kuhusu Ushirikishwaji wa Umma wa 2019 uliowasilishwa kwa mara ya kwanza katika Seneti na aliyekuwa Seneta Maalimu Haji Farhiya.

Mswada huo unatoa mwongozo kuhusu namna ya kushirikisha umma katika maamuzi muhimu.

Mswada huo ukipitishwa kuwa sheria utamaliza ujanja wa wanasiasa kukutana katika mahoteli ya kifahari na kisha kuandaa ripoti hata bila wananchi kujitokeza kutoa mapendekezo yao.

You can share this post!

Mpango fiche wa Ruto kuzamisha jahazi la Azimio

WANDERI KAMAU: Lilikuwa kosa kuwaogofya wanafunzi wa Gredi...

T L