• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
TAHARIRI: Bodi iziondoe dawa hatari hospitalini

TAHARIRI: Bodi iziondoe dawa hatari hospitalini

Na MHARIRI

UGATUZI ulipoanza kutekelezwa mwaka 2013, mojawapo ya sekta zilizogatuliwa ni ile ya afya.

Huenda hekima ya waliotunga marekebisho ya Katiba ilikuwa kwamba, wananchi watahudumiwa vyema kiafya iwapo huduma za matibabu zitasimamiwa katika ngazi ya kaunti.

Magavana wengi walianzisha zahanati, wakajenga hospitali na zile zilizokuwapo zitapandishwa ngazi. Kwa mfano katika kaunti kama Kiambu, kuna hospitali ya Rufaa ya Kenyatta, hospitali za ngazi za sita, tano na hadi chini kabisa.

Hali hii inashuhudiwa katika karibu kila kaunti nchini ambapo sasa wananchi wanafurahia kupata matibabu kwa urahisi. Kinyume na zamani ambapo wagonjwa wangeandikiwa kwenda Hospitali Kuu ya Kenyatta, Nairobi, wengi sasa hufanyiwa upasuaji au kutibiwa maradhi sugu wakiwa katika kaunti zao.

Hata hivyo, ufichuzi wa Bodi ya Dawa na Sumu (PPB) kwamba kaunti zote 47 zinahifadhi dawa ambazo muda wake wa kutumika umeisha ni tisho kwa afya ya wananchi.

Bodi hiyo inasema isipokuwa Taita-Taveta na Kajiado ambazo zimetuma maombi ya kuruhusiwa kuzitupa dawa zilizoharibika, nyingine 45 zimenyamaza bila ya kueleza juhudi zinazofanya kuziondoa hopsitalini.

Kuwepo dawa hizi kunaibua maswali kuhusu usimamizi wa kaunti. Mara kwa mara magavana kupitia Baraza la Magavana (CoG) wamekuwa wakilalaminia Shirika la Serikali la Utoaji Dawa (KEMSA) kwamba hawajapewa dawa.

Inakuaje baada ya kupewa dawa hizo, hazitumiwi hadi ziharibike? Je, ina maana kuwa kaunti huagiza dawa nyingi kupita kiasi? Au madaktari katika hospitali za kaunti wanaendelea kuwatuma wagonjwa kununua dawa katika maduka? Ni kwamba wananchi wameimarika kiafya hadi hawahitaji dawa hospitalini?

Magavana pia wanapaswa kufuatilia kwa makini na kuelewa chanzo hasa cha dawa hizo kutotumika? Mawaziri wa Afya wa kaunti watoe ripoti kamili kuhusu kilichosababisha dawa kutotumiwa kwa muda unaohitajika.

Inaeleweka kuwa wakati wa Covid-19 watu wengi hawakuwa wakienda kutafuta tiba katika hospitali. Wakati huo, magavana na maafisa wengine wakuu wa kaunti wangetambua hali hiyo na kuchukua hatua mapema.

Kamati ya Afya ya Seneti chini ya Seneta Michael Mbito yapaswa kufuatilia suala hili kwa haraka. Kamati ihakikishe kuwa dawa zote zilizoharibika zinaondolewa kutoka hospitali za kaunti.

Aidha, magavana waagizwe kununua dawa nyingine kwa kiwango kinachohitajika, ili wananchi wasitibiwe na kupewa dawa zinazoweza kuwadhuru.

You can share this post!

WANTO WARUI: Tofauti baina ya walimu na mwajiri wao...

Warembo waangushana kuona kiongozi wa vijana akiwa na gari

T L