NA MHARIRI
KILA Juni 14, ulimwengu huadhimisha Siku ya watu kuchangia damu duniani. Mwaka huu, kaulimbiu ilikuwa “Utoaji damu ni suala la pamoja. Tuungane, tuokoe maisha.”
Kauli mbiu hii ilikuwa muafaka, ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu, serikali kupitia wizara ya Afya imekuwa ikiwalilia Wakenya wajitokeze kwa wingi kutoa damu.
Tangu enzi za Waziri wa Afya Charity Ngilu, serikali imekuwa ikisikitishwa na hali ambapo Wakenya wengi hukataa kutoa damu kwa misingi ya utamaduni kati ya sababu nyingine.
Mzigo wa kutoa damu mara nyingi huwa wa wanafuzi katika shule za upili au vyuo vikuu.
Katika nchi ambapo Wakenya saba huhitaji kuingizwa damu kila baada ya dakika kumi, ni wazi kuwa kunahitajika damu ya kutosha.
Ndio maana aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Bi Sabina Chege, aliwahi kuwasilisha Bungeni mswada wa kudhibiti utoaji damu nchini.
Mswada huo Kenya National Blood Transfusion Service (LNBTS) Bill, 2020 uliungwa mkono na wabunge wengi.
Kati yao ni aliyekuwa Mbunge wa Tongaren, Dkt Eseli Simiyu, alisema kama mswada huo ungekuwa sheria, ungesaidia kuokoa maisha.
Cha kusikitisha ni kwamba, punde kipenga cha Uchaguzi mkuu kilipopulizwa, mswada huo ulisahauliwa na ukapitwa na wakati.
Takwimu za Shirika la Huduma za Utoaji Damu (KNBTS) zinaonyesha kuwa mwezi Juni mwaka huu serikali ilikuwa imekusanya panti 175,000 za damu ikilinganishwa na mahitaji ya panti 500,000.
Ina maana kuwa kulikuwa na uhaba wa panti 325,000 za damu, na hali huwa ngumu zaidi wanafunzi wanapoenda likizoni kama sasa hivi.Kwa hivyo inaudhi kusikia ripoti ya Mkaguzi wa Serikali ikisema kuwa panti 12,044 za damu zilitupwa kwa kuharibika au sababu nyingine zinazoweza kuepukika.
Dkt Nancy Gathungu alieleza Bunge kuwa zaidi ya 6,000 zilitupwa kwa kuwa na maambukizi. Nyingine 5,685 zilikusanywa kutoka kwa watu waliokuwa na uzani wa chini au wa uzito kupita kiasi.
Vile vile, panti 382 ziliharibika kwa kupitisha muda wa ubora wake. Sababu kuu inayochangia haya ni eti KNBTS haina vifaa vya kusafirishia au kuhifadhia damu.
Kwa hivyo inapofika vituoni huwa imeharinika.
Shirika hili linalosimamiwa na Dkt Nduku Kilonzo lina umuhimu mkubwa katika kuokoa maisha ya watu wanaokimbizwa hospitalini wakihitaji damu kwa dharura.
Serikali ilipaswa kuurejesha upya mswada wa Bi Chege, ili masuala yanayohusu usafirishaji na utunzaji wa damu yashughulikiwe kisheria.
Kuendelea kuruhusu damu iharibike bila kuwafaa wagonjwa, kunaweza kuwavunja moyo Wakenya wachache wanaojitolea kuchangia damu kila mara.