• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
TAHARIRI: FKF ichunguze malalamiko yanayoibuliwa kuhusu marefa viwanjani

TAHARIRI: FKF ichunguze malalamiko yanayoibuliwa kuhusu marefa viwanjani

NA MHARIRI

WAKATI huu msimu wa soka nchini unaelekea kumalizika, itakuwa vyema iwapo waamuzi wa mechi hizo watatekeleza wajibu wao bila kupendelea.

Tumeanza kusikia na kushuhudia malalamiko kutoka kwa baadhi ya timu zinazoshiriki kwenye ligi mbali mbali zikidai kwamba zinaonewa hadharani, zikishuku kwamba huenda waamuzi wameanza kuchukuwa rushwa. Imekuwa kawaida kwa malalamiko kama hayo kutokea kila msimu unapoelekea ukingoni na tuhuma hizi zimekuwa zikijirudia kila msimu.

Timu nyingi zimekuwa zikilalamika hasa zinapocheza mechi za ugenini, zikidai kwamba baadhi ya viongozi wa timu za nyumbani wamekuwa wakishawishi matokeo mazuri kwa timu zao.

Baadhi ya viongozi wa timu za ligi wamedaiwa kutumia rushwa ili timu zao zipate mwanya wa kushinda timu nyingine na kupanda daraja.

Mbali na waamuzi wa mechi kulaumiwa, vile vile kumekuwa na madai kwamba baadhi ya wachezaji wanatumiwa kuuza mechi ili wafaidike kifedha. Haya ni madai mazito ambayo yanastahili kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Zamani wasimamizi wa kabumbu nchini walihakikisha ukweli unatendeka viwanjani, na aliyepatikana na makosa kuadhibiwa vikali.

Wengi wanafurahia kuona ligi zetu zikiwa na upinzani mkali, na washindi kupatikana kwa haki, na si jinsi yanavyoendeshwa na watu wanaofurahia kuona soka ikiangamia kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Ni jukumu la Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kutafuta njia ya kuondoa kabisa dhana ya waamuzi kupokea bahasha ili wasaidie baadhi ya timu zinazotaka kupata matokeo kwa njia ya mkato, badala ya uwanjani hadharani.

Msimu huu, Wakenya wameshuhudia mechi kadhaa zikitibuka katika viwanja mbalimbali wakati wa mechi za ligi tofauti, jambo ambalo limeshusha sifa ya taifa katika mchezo huu unaopendwa na wengi kote duniani.

Baada ya visa hivyo kutokea, hakuna uchunguzi wowote wa kina uliofanywa ili wahusika waadhibiwe. Imekuwa vigumu kwa timu kadhaa kushindwa kupata ushindi hasa ugenini kutokana na rushwa ambayo imeenea kote.

Kwenye ligi za mataifa jirani kama Tanzania na Uganda, timu ikipatikana kujihusisha na rushwa huchukuliwa hatua kali ya kinidhamu.

Iwapo hali hii itaendelea miongoni mwa timu zetu, soka yetu itaporomoka na nchi itakuwa ikipata wawakilishi bandia ambao watakuwa wakibanduliwa mapema katika mashindano ya ya CAF.

Wakati tabia hii inazidi kupamba, kuna wale wanaofaidika, lakini kwa jumla tutajipata hatarini iwapo dhuluma hii haitazimwa haraka.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Waafrika watafute mbinu za kusuluhisha...

Baraza la kusimamia biashara ya vyuma chakavu laonya...

T L