• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
TAHARIRI: FKF iingilie mzozo kati ya makocha Aussems, Matano

TAHARIRI: FKF iingilie mzozo kati ya makocha Aussems, Matano

NA MHARIRI

MAKOCHA nchini wanastahili kuheshimiana na kuwa kielelezo bora kwa wachezaji wao na wale ambao wangependa kujihusisha na taaluma hiyo.

Kwa wiki mbili sasa kumekuwa na uhasama mkubwa kati ya kocha wa AFC Leopards raia wa Ubelgiji Patrick Aussems na mwenzake wa Tusker Robert Matano kuhusiana na matokeo ya mechi kati ya timu hizo iliyosakatwa mnamo APrili 5. Tusker ilishinda mechi hiyo 1-0 baada ya kufunga bao dakika za jioni.

Hata hivyo, kile ambacho kilizua uhasama ni madai ya Aussems kwamba Matano anatumia nguvu za giza kushinda mechi za Ligi Kuu (KPL). Akitumia akaunti yake ya Twitter, Aussems alimrejelea Matano kama mkufunzi mkongwe ambaye hana uzoefu wowote akilinganishwa naye.

Kufikia jana, Matano kupitia kampuni moja ya uwakili nchini alikuwa amemwaandikia Aussems barua ya kumpa siku tatu amwombe msamaha la sivyo wakutane kortini ambapo atamshtaki kwa kumharibia jina na sifa.

Iwapo kesi hiyo itafikia mahakamani, hii itakuwa mara ya kwanza ambapo kocha anayeshiriki Ligi Kuu (KPL) atakuwa akishtakiwa kortini na mwenzake. Hilo halijawahi kutokea kwenye historia ya nchi.

Kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria cha 67 kinachozungumzia Ushirikina, mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kutumia uchawi, atafungwa miaka mitano gerezani. Kifungu hicho kinazungumzia uchawi kama kinachosababisha uoga au kutumia nguvu za giza ambazo hazieleweki kufanikisha jambo.

Hata hivyo, kibarua kigumu ni kuthibitisha uchawi huo na hilo ndilo atakalokumbana nalo Aussems iwapo hatamwomba Matano msamaha kufuatia makataa hayo ambayo yanakamilika leo. Iwapo suala hilo litafikia kortini basi hatakuwa na jingine ila kuthibitisha madai hayo.

Hata hivyo, ni vyema hili suala la Aussems na Matano halikustahili kufika hapa iwapo makocha wangekuwa wakiheshimiana. Hili jambo limeibua dhana kwamba makocha wa kigeni wanawadharau wenzao wa hapa nchini jambo ambalo halistahili kamwe.

Shirikisho la Soka Nchini (FKF) nalo limekimya kuhusu suala hili wala halijachukua hatua kuhusu masuala yenye utata ambayo huibuka kila mara. Je, kazi ya shirikisho ni nini iwapo litawaacha makocha wakipapurana hadharani bila kuthamini maadili.

Katika mafunzo ya ukocha kuna masuala yanayofundishwa hasa maadili na nidhamu. Hata hivyo, hii mikwaruzano kati ya Aussems na Matano yaonyesha kinyume na kutoa mfano mbaya kwa wakufunzi ambao wanaibukia.

FKF linastahili kuwa sehemu ya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya makocha ambao wanalumbana badala ya kuwacha suala hilo lifike kortini. Hii si mara ya kwanza ambapo shirikisho linakosa kuwajibika hasa kuhusu masuala yanayopaka soka ya Kenya tope.

  • Tags

You can share this post!

Europa League: Man-United walivyotupa uongozi na kutoka...

DOUGLAS MUTUA: Wakenya waliofungwa jela Uganda hawafai...

T L