• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
TAHARIRI: Gor, Tusker hazikufaa kubanduliwa kombe la CAF

TAHARIRI: Gor, Tusker hazikufaa kubanduliwa kombe la CAF

KITENGI cha UHARIRI

MASHABIKI wa soka nchini walikumbwa na masikitiko tele baada ya timu mbili za Kenya kuondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Mashirikisho (CAF) iliyopita.

Licha ya wengi kujawa na matumaini kwamba angalau kikosi kimoja kingetamba na kusonga kwa kiwango cha juu, mambo yalienda kombo wakati timu hizo zilizoangushwa na kuaibishwa na timu za Tunisia na Congo Brazzaville.

Linalouma mashabiki wengi moyoni ni madhara ambayo kushindwa huku kutaigharimu taifa letu. Kwanza viwango vya soka vinatarajiwa kushuka kutoka nambari ya sasa ya 106 duniani kulingana na misimamo ya Fifa na kwenda chini.

Pili, hamasa na ari ya soka kwa vijana wetu itadorora na kufanya wakose ukakamavu katika fani hii. Vivyo hivyo, wachezaji watakosa imani na wakufunzi na usimamizi wa soka nchini kwa jumla. Ingawa si uungwana kulaumu vikosi vyetu kwa kuwa, asiyekubali kushindwa si mshindani, ni sharti maswali ya kushindwa kwao yajibiwe ili kuzuia tukio kama hili kujirudia siku za usoni.

Klabu ya Tusker FC ina kila uwezo wa kufanya vyema kutokana na uwezo wake wa kifedha kwani udhamini wao ni dhabiti. Hii ni timu ambayo ina vifaa vya kutosha na wachezaji wake hulipwa vizuri bila kucheleweshwa mishahara na marupurupu kama baadhi ya klabu nyingine humu nchini.

Kwa sababu hii kocha Robert Matano alifaa kujikaza kuiweka imara safu ya wasakataji wake kuzuia aibu kama hii kutokea. Kosa ambalo alifanya ni kutimua vifaa 14 na kusajili wengine 15 muda mchache kabla ya kipute hiki kuanza.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba vijana hawa wapya hawakuwa wamezoeana vya kutosha kucheza pamoja. Pia, mkufunzi huyu anafaa kuimarisha uhusiano bora zaidi kati yake na vijana wake ili mawasiliano yawe bora zaidi.Ni muhimu pia apange mikakati ya kukabiliana na timu za Kaskazini mwa Afrika ambazo amezoea kukumbatia vichapo kila wakati anapokutana nazo.

Matano afaa kujipanga vile atafuta rekodi hii ya kufedhehesha kwa dharura.Kwa upande wa Gor Mahia, ni sharti ieleweke kuwa klabu hii ilikabiliwa na matatizo ya kifedha kutokana na ufadhili finyu. Baadhi ya wachezaji wake walilalamikia kukosa mishahara na marupurupu.

Pia idadi ya wachezaji wake ilikuwa 16 na pekee jambo lililochangiwa na adhabu ya Fifa baada ya kushtakiwa na wachezaji wake wa zamani kwa kutowalipa.Ni muhali usimamizi wa timu hizi ujifunze kutokana na upungufu kuzuia kushindwa tena siku za usoni. Ushindi ni fahari ya taifa nzima si kwa mashabiki na wamiliki klabu pekee.

You can share this post!

Ni mguu niponye pasta akifuata waumini kwa mama pima...

WANDERI KAMAU: Idadi ya polisi wenye matatizo ya afya ya...

T L