NA MHARIRI
MAMIA ya watu waliotoa huduma kwa taasisi za serikali wanaendelea kuhangaika.
Biashara zao zimeathirika. Wengi wamekuwa wa kujificha na kutoroka wanaowadai, kwa sababu ya kutolipwa ujira wao kama walivyokubaliana na idara za serikali.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha jinsi ambavyo serikali ya taifa au zile za Kaunti, zimekuwa zikiwapa kandarasi au kupokea huduma kutoka kwa watu na kampuni, kisha kuwahangaisha wakati wa malipo.
Mojawapo ya ripoti hizo zinaonyesha jinsi wanakandarasi waliojenga madarasa 10,000 ya kufanikisha Mtaala Mpya wa Masomo (CBC) wanavyoandamwa na kampuni za mnada.
Kulingana na wanakandarasi hao, walistahili kupokea malipo yao mwezi Agosti 2022. Inaonekana siasa za kampeni ziliwasahaulisha wakuu serikalini na kukosa kuwalipa watu hao hadi leo.
Kuna ripoti kuhusu kampuni moja iliyopewa kandarasi ya kujenga ukuta katika gereza la la Mandera. Tangu mwaka 2016, mwanakandarasi aliyekamilisha kazi yake alilipwa Sh2.5 milioni pekee. Ingawa alilazimika kukopa ili kukamilisha ukuta huo, hadi leo hawajalipwa pesa zilizobaki.
Akurugenzi wa kampuni husika wameshindwa kuwalipa wafanyikazi wao na watojai huduma wengine.
Kitu ambacho serikali haitambui ni kuwa, wanakandarasi wengi hulazimika kuchukua mikopo ili kukamilisha miradi haraka. Walifanya hivyo kwa sababu serikali ilikuwa imeahidi kulipa ndani ya miezi miwili. Sasa baada ya kusubiri tangu Agosti 2022 au zamani zaidi, hakuna ambaye amewasiliana nao kuhusu lini watapokea pesa zao.
Mtindo huu wa kutoa kandarasi kwa watu na kunyamaza kuhusu malipo sio tu ukiukaji wa sheria za kandarasi, bali unawaweka wanakandarasi katika hali ngumu. Kumekuwa na ongezeko la visa vya watu kujitoa uhai kwa sababu ya kusukumwa ukutani na mambo kama haya.
Wakuu wanaohusika na utoaji kandarasi anapaswa kujipanga vyema na kutenga pesa kabla ya kutafuta huduma.
Kwenye kandarasi za ujenzi wa madarasa, wanakandarasi wengi waliotumika ni watu wadogo, wasiokuwa na uwezo wa kifedha kuwalipa waliowapa vifaa. Waliowapa kazi ya kukoroga saruji, kusaidia kubeba zege na kadhalika, wana mahitaji yao muhimu.
Wakati huu ambapo kila mtu anakabiliwa na ugumu wa maisha, ni vyema kwa idara za serikali kutimiza ahadi zake na kukamilisha malipo. Serikali daima zitahitaji huduma.
Jambo la busara ni kuwalipa kwa wakati wanaotoa huduma hizo, ili wawe na uwezo wa kutoa huduma zaidi siku za mbeleni.