• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
TAHARIRI: KCPE: Serikali itatue lalama kuhusu matokeo

TAHARIRI: KCPE: Serikali itatue lalama kuhusu matokeo

NA MHARIRI

BAADHI ya shule nchini zimejitokeza na kupinga matokeo ya Mtihani ya Darasa la Nane (KCPE) yaliyotangazwa Jumatano na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Miongoni mwa shule zilizotilia shaka matokeo hayo ni Inyokono iliyoko katika Kaunti ya Makueni na Kitengela International School ya Kaunti ya Kajiado.

Mathalani, watahiniwa 82 kati ya 124 wa shule ya Inyokono, walipata alama 400 na zaidi katika mtihani wa mwaka 2021. Aliyepata alama za chini mwaka huo alikuwa na alama 352 kati ya 500.

Lakini matokeo yaliyotangazwa na Waziri Machogu Jumatano yaliacha walimu na wanafunzi vinywa wazi baada ya mwanafunzi bora kupata alama 352 pekee.Watahiniwa waliokuwa wakipata alama 400 na zaidi katika mitihani ya majaribio walijipata na alama 200 katika mtihani wa KCPE.Wanafunzi 170 wa shule ya Kitengela International walipigwa na butwaa baada yao kukosa kufikisha alama 400.

Watahiniwa 40 waliofanya KCPE katika tawi la shule hiyo lililoko katika eneo la Syokimau, Kaunti ya Machakos, pia waliathirika kwani hamna aliyepata alama 400; wengi wa watahiniwa walipata alama zisizozidi 350 huku wengi wao wakipata chini ya alama 300.

Usimamizi wa shule hiyo umeshikilia kuwa hakukuwa na visa vya udanganyifu shuleni hapo wakati wa kufanya mtihani.

Malalamishi sawa na hayo pia yamekuwa yakitolewa na shule nyingine nchini ambazo matokeo yake yalidorora mwaka huu licha ya kufanya vyema miaka iliyopita.

Kumekuwa na ripoti katika vyombo vya habari kwamba baadhi ya wanafunzi walizimia baada ya kupata alama za chini ambazo hawakutarajia.

Ni kawaida kwa shule iliyofanya vyema katika mitihani ya kitaifa mwaka fulani na kisha kuporomoka mwaka unaofuatia. Kuna shule nyingi ambazo zilikuwa zikiwika zamani katika mitihani ya kitaifa lakini sasa zinang’ang’ana hata kupata mwanafunzi anayefikisha alama 250 kati ya 500.

Hata hivyo, malalamishi ya shule zinazotilia shaka matokeo ya mwaka huu 2022 hayafai kupuuzwa – Wizara ya Elimu haina budi kuyachukulia kwa uzito.

Wakati wa kutangaza matokeo hayo Waziri Machogu alisema kuwa kila shule itapewa ripoti yake ya kina kuhusiana na matokeo ya KCPE ya 2022 Januari 2023.

Ripoti hiyo itasaidia pakubwa kuhakikisha kuwa shule zilizo na dukuduku zinaridhika.

Serikali ilifaa kutoa ripoti hiyo pamoja na matokeo ili kuondolea dukuduku shule ambazo hazijaridhika. Kucheleweshwa kwa ripoti hiyo hadi Januari kunaongeza shaka na uvumi.

You can share this post!

Kaunti yaanza matayarisho ya Madaraka Dei

DOMO: Ni kweli hana haya

T L