• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
TAHARIRI: Maandamano: Sheria ifuatwe

TAHARIRI: Maandamano: Sheria ifuatwe

NA MHARIRI

MAANDAMANO ya Upinzani yanayotarajiwa kufanyika leo katika baadhi ya maeneo nchini, yameibua hisia mseto – yameungwa mkono na kukashifiwa kwa kiwango sawa.

Baadhi ya viongozi wa makanisa, wanasiasa na wafanyabiashara wamelaani maandamano ya leo wakisema kuwa yatavuruga biashara na kuchochea uhasama nchini.

Wanaounga mkono wanasema kuwa maandamano hayo ni muhimu katika kushinikiza serikali kupunguza gharama ya juu ya maisha.

Jana Jumapili, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi Adamson Bungei, alitaja maandamano hayo yanayoongozwa na kinara wa Azimio Raila Odinga kama ‘haramu’.

Bw Odinga amewataka wafuasi wake kukusanyika katikati mwa jiji la Nairobi na kisha baadaye kufululiza hadi Ikulu.

Kwa mujibu wa Bw Bungei, maandamano ya Azimio ‘hayajatimiza vigezo’, hivyo hayataruhusiwa.

Saa chache baadaye, Waziri wa Usalama Profesa Kithure Kindiki alionekana kupuuzilia mbali kauli hiyo ya Bw Bungei kwa kusema kuwa wataheshimu haki ya kikatiba ya Wakenya watakaoshiriki maandamano lakini polisi watazuia waandamanaji kuingia katika baadhi ya maeneo kama vile Ikulu, kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo yenye Ulinzi Mkali.

Ukweli ni kwamba Kifungu cha 37 cha Katiba kinawapa Wakenya wote haki ya kuandamana almradi hawajajihami kwa silaha.

Raia hawahitaji kuomba ruhusa kwa polisi kutekeleza haki yao ya kuandamana; bali watu wanaohitaji kuandamana wanafaa tu kuwafahamisha polisi kuhusu mpango wao ili wapewe ulinzi.

Hivyo, kauli ya Bw Bungei kwamba maandamano ya Azimio hayajakidhi baadhi ya matakwa, inapotosha. Polisi hawana mamlaka ya kutathmini ni maandamano yapi yametimiza vigezo na yapi hayajatimiza ili kutoa idhini au kukataa.

Maafisa wa polisi wamekuwa wakishutumiwa kwa ‘kuchokoza’ waandamanaji na kusababisha vurugu.

Mara baada ya kuapishwa kushika hatamu za uongozi Rais William Ruto alitangaza kuwa hatatumia polisi kuendeleza ajenda za kisiasa. Hivyo, maafisa wa polisi hawana budi kutoa ulinzi kwa waandamanaji leo Jumatatu.

Kwa upande mwingine, waandamanaji wanastahili kufuata sheria wanapoandamana kushinikiza serikali kupunguza gharama ya bidhaa kati ya matakwa mengineyo.

Japo Katiba inaruhusu maandamano, inapiga marufuku waandamanaji kubeba silaha, kuzua rabsha, kusababisha uharibifu wa mali na kutatiza shughuli za watu.

Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia waandamanaji wakisababisha uharibifu wa mali na hata umwagikaji wa damu.

Bw Odinga na viongozi wenzake wa Azimio wana kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa maandamano ya leo Jumatatu yanazingatia Katiba.

Waandamanaji waepuke uharibifu wa mali na hata kutatiza shughuli za kila siku mijini.

  • Tags

You can share this post!

Ni roho mkononi maandamano yakiitikisa dunia

Maandamano: Shughuli za kawaida zapungua jijini Nairobi...

T L