• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
TAHARIRI: Magavana waipe miradi ya maendeleo umuhimu

TAHARIRI: Magavana waipe miradi ya maendeleo umuhimu

NA MHARIRI

MAGAVANA wapya 28 walipochaguliwa mwaka 2022, kulikuwa na matumaini tele kwamba wangeleta mabadiliko ambayo wapigakura wamekuwa wakitamani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi.

Matumaini ya ustawi katika kaunti yalikuwa juu zaidi kwani wengi wa magavana hao wapya ni vijana.

Magavana hao walianza muhula wao wa kwanza kwa kishindo huku baadhi yao wakiunda majopokazi ya kuchunguza jinsi watangulizi wao walitumia fedha za umma.Uchunguzi huo ulifichua uozo wa kila aina katika kaunti mbalimbali.

Katika Kaunti ya Siaya, kwa mfano, uchunguzi ulifichua jinsi serikali ya aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo, Cornel Rasanga, ilitumia Sh285 milioni kununua chai wakati wa semina ilhali sekta za afya na kilimo zikidorora kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha.

Uchunguzi uliofanywa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) ulifichua wafanyakazi hewa 1,300 ambao walikuwa wakilipwa mishahara minono katika Kaunti ya Kisii chini ya uongozi wa Bw James Ongwae aliyestaafu baada ya kukamilisha mihula yake miwili.

Katika kaunti jirani ya Migori wafanyakazi hewa 600 walikuwa wakilipwa mamilioni ya fedha chini ya Bw Okoth Obado aliyekamilisha mihula yake miwili mwaka 2022.

Katika mkutano wa hivi karibuni, magavana walipokutana mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru, walilalamikia uwepo wa wafanyakazi hewa kama changamoto kuu inayosababisha fedha za kaunti kupotea. Wizi huo wa fedha za kaunti kupitia kwa wafanyakazi hewa, unasabisha miradi ya maendeleo kukwama kwa kukosa hela. Lakini ripoti ya hivi karibuni Mkaguzi wa Matumizi ya Fedha za Umma Margaret Nyakang’o, inayoonyesha kuwa wengi wa magavana wanaohudumu muhula wa kwanza hawana tofauti na watangulizi wao – wametelekeza miradi ya maendeleo.

Sheria inahitaji kuwa asilimia 30 ya fedha za kaunti zielekezwe katika miradi ya maendeleo. Lakini ripoti ya Bi Nyakang’o imebaini kwamba magavana wote wapya wameshindwa kutekeleza sheria ya kutenga asilimia 30 ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Ripoti hiyo, kwa mfano, inasema kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii chini ya Gavana Simba Arati, inatumia karibu fedha zote katika kulipa mishahara, kununua mafuta ya magari na kurembesha au kukarabati maofisi. Kinaya ni kwamba Kaunti ya Kisii imekuwa katika mstari wa mbele kupambana na wafanyakazi hewa na maafisa wafisadi.

  • Tags

You can share this post!

Kanisa lakosoa vikali mahakama kwa uamuzi tata kuhusu...

Bonde laibukia kuwa ngome maarufu ya pombe bandia

T L