• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
TAHARIRI: Malipo mazuri kwa marefa ndiyo dawa ya usimamizi duni wa mechi

TAHARIRI: Malipo mazuri kwa marefa ndiyo dawa ya usimamizi duni wa mechi

NA MHARIRI

KATIKA kipindi cha siku 10 hivi zilizopita, suala kuu la uadilifu miongoni mwa marefa limejitokeza katika matukio yanayozidi matatu.

Mojawapo ya mechi zilizoangaziwa zaidi zinajumuisha kipute cha ligi kuu baina ya Bandari na City Stars ambapo refa aliongeza dakika 15 kisha akawatuza wenyeji hao penalti.

Mechi kubwa kati ya Gor Mahia na Tusker pia ilizua maswali baada ya Gor kupewa penalti ya kutiliwa shaka.

Vilevile malalamiko yalihusu timu za ligi ya kitaifa ya NSL na ligi za kinadada.

Suala jingine ni ukosefu wa uadilifu miongoni mwa wachezaji.

Wiki hii wachezaji 15 wamepigwa marufuku baada ya kuhusishwa na upangaji wa mechi.

Upangaji huo unaonekana kuchangiwa na ama malipo mabovu au upujufu wa maadili miongoni mwa wanasoka wetu pamoja na wanamichezo wengine.

Katika uchunguzi wetu wa awali, imebainika kuwa marefa na wachezaji wa Kenya wanalipwa ‘pesa-nane’.

Wengine hucheleweshewa malipo ama hata kukosa kuyapata malipo hayo kabisa. Katika hali kama hiyo, marefa wanajipata katika vishawishi vya ama kupendelea klabu au timu moja inayotoa rushwa, na kwa kiwango fulani hata kushiriki katika kamari ya spoti.

Waamuzi wa soka wana mchango mkubwa katika kudumisha uadilifu huo, kuhakikisha kwamba mechi zinachezwa kwa haki na kwa mujibu wa sheria.

Kwa bahati mbaya, suala la upangaji wa matokeo na upendeleo linaendelea kuathiri mchezo huu hasa nchini Kenya, na ni wakati mwafaka kwetu kuchunguza upya suala mishahara ya waamuzi.

Ikizingatiwa kuwa waamuzi mara nyingi hukabiliwa na shinikizo kubwa hasa kutoka kwa mashabiki, wachezaji na makocha wanaotaka maamuzi ya busara na haraka mechi inapoendelea, ni aula shirikisho la soka la Kenya (FKF) liingilie kati katika juhudi za kuhakikisha kuwa wanalipwa vizuri na kwa wakati ufaao.

Vinginevyo, mapendeleo, rushwa na upangaji mechi havitaisha nchini.

Mwamuzi anayelipwa vizuri hakabiliwi na shinikizo kubwa la kupokea hongo au kushawishika na vishawishi vinginevyo mbalimbali kama vile kupanga mechi ili ashinde beti au kamari ya mchezo.

Ikiwa tunataka kushughulikia suala la upangaji wa mechi na upendeleo, lazima tuhakikishe kuwa waamuzi wanalipwa vizuri kwa kazi yao.

Mshahara unaostahili utasaidia kupunguza rushwa na kuunda mazingira mazuri zaidi ya kazi ya uamuzi wa mechi.

Mustakabali wa mchezo huu unategemea hatua hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Shughuli za uokoaji wa wachimba migodi 2 Sigalagala...

Korti yazuia Waititu kusafisha mito ya Nairobi

T L