• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
TAHARIRI: Matamshi haya ya ‘kiwazimu’ sharti yazimwe

TAHARIRI: Matamshi haya ya ‘kiwazimu’ sharti yazimwe

NA MHARIRI

KATIKA demokrasia nyingi zinazostawi, wanasiasa wanaojiona kuwa karibu na utawala hujisahau na kupita mipaka yao.

Hujiona kama wenye mamlaka mengi na hatimaye kuanza kuyatumia vibaya. Mnamo Jumatatu, Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Bw Aaron Cheruiyot aliwakumbusha wengi kuwa yeye, ‘kama serikali’, ana uwezo wa kumaliza ‘maovu’ yote katika taifa hili.

Alisema makiritimba (makateli) wamejaa katika kila pembe ya Kenya na kuelezea matumaini yake kuwa utawala wa Rais William Ruto utayamaliza ‘madubwana’ hayo mahatinafsi ila tu itatatizika kuyaangamiza ‘madude’ hayo katika sekta ya uanahabari na benki.

Aliongeza kuwa hata ingawa makiritimba wa sekta hizi mbili ni wagumu kuangamizwa, hatimaye watamalizwa tu. Naam, huenda ni kweli makiritimba yamejaa kila pembe ya nchi ila katika uanahabari, seneta huyo alikosea.

Unapotafakari kuhusu asili ya mtazamo wa seneta huyo, unabaini kuwa unatokana na serikali kutoangaziwa kwa uzuri na vyombo hivyo.

Kama mmoja wa watetezi wa serikali ya Kenya Kwanza, huenda anahofia kuwa serikali inapokosolewa na vyombo vya habari kwa kutofanya baadhi ya mambo ipasavyo, huenda hilo likamsawiri Rais kama asiyeweza kazi ya kuiendesha nchi, hivyo basi, kumkosesha kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Seneta Cheruiyot anasahau kuwa kati ya asasi zinazofaa kuikosoa serikali zaidi ni upinzani na vyombo vya habari. Ukosoaji huendeshwa na wanahabari kwa kufuata kanuni zilizopo za uwazi, kutopendelea au kutoshambulia mtu au taasisi yoyote kwa nia mbaya ya kibinafsi.

Duniani kote, vyombo vya habari hutekeleza jukumu kubwa la kuikosoa serikali ili iepuke utawala mbaya unaoweza kuitumbukiza nchi pabaya kisiasa, kiuchumi au kijamii.

Labda Bw Cheruiyot alisema hayo ili vyombo vya habari viogope kuipiga serikali darubini. Hilo halitawezekana. Kadri serikali inavyoenda kinyume na utawala bora, ndivyo itakavyomulikwa kwa ubaya.

Nguzo kuu ya utawala bora ni kutunga sera nzuri za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Yaani serikali iwape raia wa kawaida umuhimu badala ya kuzama katika kutimiza maslahi ya kibinafsi.

Matokeo mazuri kiuchumi, kiutawala na kijamii yatakapoanza kuonekana, seneta huyo awe na hakika kuwa hakuna chombo cha habari kitakachoendelea kuishambulia serikali yake.

Lakini iwapo bado raia wanateseka au kuteswa jinsi ilivyo kwa sasa ilhali wanaendelea kutozwa ushuru, hawezi kuepuka habari zisizo nzuri kwenye magazeti, runinga, redio na mitandaoni.

Wala si Cheruiyot pekee aliyevishutumu vyombo vya habari kwa kutekeleza jukumu lake, hata Naibu Rais Rigathi Gachagua amepatikana katika utando huo. Sharti matamshi kama hayo yanayodhihirisha hila dhidi ya vyombo vya habari yakomeshwe.

  • Tags

You can share this post!

‘Nilishinikizwa kuipa serikali ya Jubilee Sh55...

Wahadhiri wapata ujuzi zaidi wa masuala ya kiteknolojia...

T L