• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
TAHARIRI: Matamshi ya Msimamizi wa Bajeti hayakufaa

TAHARIRI: Matamshi ya Msimamizi wa Bajeti hayakufaa

NA MHARIRI

KAULI ya Msimamizi wa Bajeti bungeni kwamba alilazimishwa kuruhusu matumizi ya Sh15 bilioni na utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta inaibua maswali kuhusu utendakazi wa afisi yake.

Bi Margaret Nyakang’o aliliambia bunge eti alilazimishwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha Ukur Yatani, aruhusu pesa hizo haraka, la sivyo “apigiwe simu na rais”.

Kauli yake hiyo inazua mambo mawili: Kwanza, kwamba ni afisa wa serikali aliye na afisi huru lakini hawezi kufanya maamuzi bila ya kupokea maagizo. Pili, kwamba kuna uwezekano pesa hizo zilihitajika kwa malengo yasiyokuwa ya maendeleo ya nchi.

Wabunge wa chama cha UDA wamechukua kauli hii ya pili na kuanza kueneza propaganda kwamba, kuna pesa zilizobebwa kwa magunia na helikopta wakati huo. Bw Yattani jana alijitokeza kufafanua kuwa pesa hizo zilihitajika haraka kwa sababu ya miradi mikuu minne wakati huo.

Kwanza kulikuwa na pesa za kulipa kampuni za mafuta kwa kutoa ruzuku ya bei kwa wateja. Pili ni kampuni za kusaga mahindi, zilizokuwa zimekubaliana na Rais Mstaafu Kenyatta kuuza unga kwa bei ya Sh100.

Pia kulingana na Bw Yatani, wakandarasi waliokuwa wakijenga barabara ya Lamu kwenda Garissa na ya Garissa kwenda Isiolo, walikuwa wamesusia kazi kwa kutolipwa ujira wao.

Ikizingatiwa kuwa barabara hiyo imekuwa ikitumiwa na magaidi na majangili kuhatarisha usalama wa nchi, ililazimu kutafuta pesa za dharura kuwalipa.

Na mwisho, pesa pia zilitakikana kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Jeshi ya KDF iliyofunguliwa majuzi na Rais William Ruto.

Sheria aliyotumia Msimamizi wa Bajeti ni Kifungu cha 223 cha Katiba, ambacho kimetumika hata majuzi wakati wa kuruhusu Bajeti ya Ziada ya Sh127.5 bilioni.

Japo lengo la kutoa kauli hiyo ya kukanganya huenda lilikuwa kujiondolea lawama, afisa huyo sasa anaandamwa na wabunge wa UDA, wanaopanga kumtimua kazini. Wabunge hao sasa wanaonekana kupata nafasi nzuri ya kumteua Msimamzi wa Bajeti wanayemtaka. Iwapo ataondolewa, Bi Nyakang’o hatakuwa wa kwanza.

Wasimamizi wa mashirika ya serikali kama vile mamlaka ya KRA, Kenya Power, Kenya Pipeline kati ya mengine, wametimuliwa. Kile ambacho hawakuwa wamepata kwa Msimamizi wa Bajeti ni sababu, na sasa imejitokeza. Mtindo huu wa serikali kuwafuta kazi watu waliokuwa katika utawala uliopita bila sababu maalumu ni utumizi mbaya wa mamlaka.

Maafisa wa Afisi Huru wanalindwa na Katiba na haifai kuwatimua bila kufuata taratibu. Kuwatafutia makosa ili waondoke haraka ni kinyume cha kanuni za kimataifa kuhusu haki za wafanyikazi.

  • Tags

You can share this post!

Mwanakandarasi ashtakiwa kwa kumchapa ‘kanjo’

JURGEN NAMBEKA: Magavana waipe kipaumbele miradi muhimu...

T L