• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:37 PM
TAHARIRI: Mazungumzo yaweke maslahi ya raia mbele

TAHARIRI: Mazungumzo yaweke maslahi ya raia mbele

NA MHARIRI

HATUA ya Rais William Ruto na kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, kulegeza misimamo yao ilikuja kwa wakati mwafaka ambapo Kenya ilikuwa inaelekea pabaya.

Kwa wiki mbili zilizopita tangu Azimio ilipoanza maandamano dhidi ya serikali ya kitaifa, kumekuwa na hasara tele ambazo zimeshuhudiwa ikiwemo vifo na uharibifu wa mali.

Hasara nyingi zilitokana na wahalifu walioingilia maandamano hayo, na vilevile polisi waliotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na wanahabari.

Ugumu wa Rais Ruto na Bw Odinga kukubaliana ulitajwa na wengi kuwa chanzo cha hasara zilizotokea, na hivyo basi pande zote mbili zikabebeshwa lawama kwa kiasi fulani.

Wawili hao ambao wote hujitambulisha kama Wakristo wa madhehebu ya kuenda kanisani Jumapili, walichagua mojawapo ya siku muhimu zaidi kwa kalenda ya Wakristo kulegeza misimamo yao ya kisiasa.

Jumapili hiyo ya mitende iliashiria mwanzo wa wiki takatifu inayoelekea kwa Pasaka na hivyo basi ni muhimu waheshimu misimamo waliyochukua kutoa nafasi ya mashauriano kwa njia ya amani.

Ijapokuwa waliweka masharti kuhusu hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa kuelekea mbele, kujitolea kwao kuanzisha mazungumzo ni hatua kubwa ya kutafuta jinsi ya kutatua changamoto za nchi kwa pamoja.

Ni matumaini yetu kuwa, wataheshimu hitaji la kutatua changamoto zinazokumba raia bila kuweka maslahi ya wanasiasa mbele.

Majadiliano yatakayofanywa yasiangazie tu masuala ya kisiasa bali pia sera na sheria zinazohitaji kurekebishwa ili kupunguzia raia gharama ya maisha.

Vigogo hao wawili pia wawe macho dhidi ya wandani wao ambao huenda wakawa na nia za kibinafsi katika michakato inayotarajiwa kuanzishwa.

Kwa mujibu wa matamshi ya baadhi ya wandani wa kisiasa wa Dkt Ruto na Bw Odinga, ni wazi kuwa kuna wale wanaohofia kutengwa iwapo vigogo hao wawili wataweka kando tofauti zao za kisiasa.

Aina hii ya wanasiasa huwa ni vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya nchi kwani wao hutazama tu vile wanavyoweza kujinufaisha kibinafsi.

Mbali na hayo, michakato aina hii iliyofanywa katika serikali zilizopita ichukuliwe kama funzo ili kuepusha athari mbaya zinazoweza kutokea baadaye.

Mazungumzo yoyote yatakayofanywa yasiishie kuongeza raia mzigo kwa njia yoyote ile, iwe ni kwa kuongeza idadi ya watumishi wa kitaifa bila msingi au kuunda majopo ambayo ripoti zao hazitawahi kutekelezwa.

Haki za raia zipewe kipaumbele iwapo kweli vinara hao wawili wamejitolea kutetea wananchi jinsi wanavyoeleza mara kwa mara.

  • Tags

You can share this post!

‘Ghost’ Mulee ndiye kocha mpya wa Gaspo Women

Wenye mizigo bandarini wakwamilia SGR

T L