• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Muda mfupi wa kulipa Hustler Fund hakika haufai

TAHARIRI: Muda mfupi wa kulipa Hustler Fund hakika haufai

NA MHARIRI

MKOPO wa Hustler Fund ulioanza kutolewa kwa wananchi wenye uwezo mdogo kimapato mnamo Jumatano huenda usiwafaidi raia jinsi ilivyokusudiwa.

Hii ni kwa sababu mbali na muda mfupi wa kulipa, kiwango cha pesa kinachotolewa ni kidogo sana wala hakiwezi kutosha kuanzisha biashara ya kumtoa mkopaji kwenye umaskini.

Muda wa kulipa mkopo huo ni siku 14 au majuma mawili. Mkopo wenyewe unatolewa kwa riba ya asilimia nane.

Labda itakuwa muhimu tuchambue sera ya ‘Bottom Up’ kwenye manifesto ya mrengo wa Kenya Kwanza kabla ya uchaguzi ndipo tubaini jinsi gani mkopo huu utakavyokosa kutimiza malengo yake kusudiwa.

Sera hiyo ililenga kuwapa Wakenya wa tabaka la chini uwezo kwa kuwafungulia njia za kujinyanyua kama vile kuimarisha biashara zao ndogondogo.

Katika kufanikisha hilo, Rais William Ruto, baada ya kutangazwa mshindi, alitangaza kuwa serikali yake itakuwa ikitenga Sh50 bilioni kila mwaka ambazo zingekopeshwa raia wa tabaka hilo kwa lengo la kujiendeleza kibiashara.

Ila katika kufanikisha hilo, ilibainika kuwa benki hazingewakopesha Wakenya mikopo kwa kuwa wengi wao walikuwa na ripoti hasi kwenye afisi ya kukadiria ulipaji mikopo almaarufu CRB.

Hapo Rais alichukua hatua kwa kuzungumza na benki ambazo zilikubali kuwaondoa Wakenya kwenye CRB.

Kuondolewa huko kuna manufaa kwa mwananchi wa kawaida kwa kuwa sasa wataweza kukopa pesa kwenye benki ili kujiendeleza kimaisha.

Hata hivyo, kwa sababu harakati ya benki kuwakopesha wananchi haiwi rahisi, Wakenya wengi walitarajia kukopeshwa hela nzuri kutoka kwa Hustler Fund ili wawekeze na kujivunia faida ambayo ingeinua maisha yao.

Lakini Jumatano, wengi walishtuka kubaini kuwa wanaweza kukopa kati ya Sh500 na Sh1,500 pekee. Hakika mkopo wa kiwango hicho hauwezi kuendesha biashara yoyote ya maana na kuleta faida katika muda wa siku 14 ndipo mkopaji alipe mtaji huo pamoja na riba yake.

Hata kama hela hizo zingekuwa zinatosha kuanzisha biashara au kupiga jeki biashara zilizoanzishwa tayari, siku 14 ni chache sana kuweza kujipa faida ya kutosha ili kuulipa na riba yake.

Mtazamo wetu ni kuwa kiwango cha chini kinachotolewa kingekuwa Sh10,000 kisha muda wa kulipa urefushwe hadi angaa miezi sita.

Katika muda huo, faida inaweza kuwa imepatikana na mkopaji kulipa mkopo huo bila tatizo.

Aidha, pesa hizi, kwa mujibu wa Kenya Kwanza kabla ya uchaguzi, zilifaa kutolewa bila riba. Lakini sasa kuna riba, tena kubwa. Je, mkopaji atanufaika au atajipata katika deni asiloweza kulipa?

You can share this post!

Wauzaji muguka washtaki kaunti

DOMO: Aisee ukiwa mzembe, nyeti ndio zitaumia!

T L