• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
TAHARIRI: Naam, sekta ya viwanda ipewe uzito

TAHARIRI: Naam, sekta ya viwanda ipewe uzito

NA MHARIRI

MNAMO Ijumaa Rais William Ruto alipozuru eneo la Magharibi mwa Kenya, alisisitiza ahadi yake ya kuhakikisha kuwa viwanda vya eneo hilo vinafufuliwa.

Rais alionya mrasimu wa kampuni ya Mumias, Rai yenye maskani makuu nchini Uganda, kuwa hatasita kumbadilisha, iwapo kusudio la kukifufua kiwanda hicho kwa manufaa ya wakulima, halitapewa umuhimu.

Dkt Ruto pia ameonekana kukariri ufufuzi wa kiwanda na kilimo cha pamba katika Kaunti ya Busia ili wakazi wa eneo hilo wajikwamue kwenye lindi la umaskini walilokwama ndani hadi sasa.

Iwapo Dkt Ruto atafulu kufufua viwanda vingi vilivyoanguka, si Magharibi mwa Kenya tu bali nchini kote, basi atakuwa ametimiza mojawapo ya ahadi muhimu zaidi alizotoa wakati wa kampeni.

Kenya inahitaji viwanda ili kupunguza tatizo la uhaba wa kazi hasa kwa vijana ambalo katika siku za hivi karibuni, limeathiri ustawi wa nchi hii kwa kiwango kikubwa.

Itakuwa vyema iwapo viwanda vingine kama vile vya kutengeneza nguo na mavazi kutokana na pamba kama vile Rivatex na Kicomi vitapewa umuhimu katika mpango wa kunyanyua uchumi wa taifa hili chini ya Ruto.

Kadhalika, viwanda kama PanPaper ambavyo vilisaidia Wakenya wengi enzi hizo kwa kuzalisha karatasi za bei rahisi, vinastahili kufufuliwa.

Ukweli ni kuwa kwa kufufua viwanda hivyo, hasa vinavyojihusisha na chakula, raia wengi watanufaika kwa njia mbalimbali kama vile kuongeza mapato kutokana na ajira katika viwanda hivyo pamoja na kujipa vyakula vya ziada.

Rais Ruto wewe ni wa kusema na kutenda.

You can share this post!

Qatar kupata faida ya Sh1.1 trilioni kwa uandalizi wa Kombe...

Raila akubali mfupa wa Ruto

T L