• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
TAHARIRI: Naibu Rais awafichue wafisadi wote

TAHARIRI: Naibu Rais awafichue wafisadi wote

NA MHARIRI

UFISADI umekuwa maradhi yanayosababisha uchumi na ustawi wa taifa letu kuendelea kudidimia, kiasi cha viongozi kufeli kushirikiana kupata tiba kamili na ya kudumu.

Madhara ya ufisadi ni Wakenya kuteseka kwa kukosa ajira, maendeleo duni, gharama ya juu ya maisha, uchumi uliosambaratika na ukabila katika ajira.

Ufisadi pia umechangia miradi mingi muhimu kukwama nchini,kucheleweshwa kwa fedha za basari zinazotegemewa na watoto maskini, na wagonjwa kukosa dawa katika hospitali za umma.

Itakuwa afueni ikiwa viongozi wanaoingia mamlakani watatia shime kupambana na adui wa ufisadi, iwe ulitekelezwa na watangulizi wao au unaendelea katika serikali ya kitaifa na za kaunti.

Hivyo, Naibu Rais Rigathi Gachagua afanye kweli kutaja wandani wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anaodai walifuja Sh35 bilioni za umma katika kipindi cha mpito.

Ushahidi huo utumiwe kuwachukulia hatua kali kisheria washukiwa wote; bora tu isiwe ni njama ya kuwaangamiza kisiasa au kulipiza kisasi, kama ambavyo imejitokeza hivi karibuni katika hatua za serikali hii mpya.

Kuwataja wafisadi tu hakutoshi bali hatua zaidi za haraka zinahitajika ikiwa serikali hii inataka kupiga jeki juhudi za ukombozi wa taifa dhidi ya jinamizi la ufisadi.

Wakenya wanafaa kuwa makini wasipotoshwe na viongozi wanaoingiza siasa katika jitihada za kung’oa mizizi ya ufisadi nchini.

Vita hivi vitafaulu tu ikiwa wote – samaki wakubwa kwa wadogo – wanaothibitishwa kuhusika watachukuliwa hatua.

  • Tags

You can share this post!

Shehena ya kwanza ya mahindi ya manjano kutua leo Jumapili

JUNGU KUU: Mipasuko yadhihirika katika Kenya Kwanza

T L