• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:20 AM
TAHARIRI: Namwamba, viongozi nchini wasaidie klabu za soka kifedha

TAHARIRI: Namwamba, viongozi nchini wasaidie klabu za soka kifedha

NA MHARIRI

MSIMU wa ligi kuu soka ya taifa FKF-PL unaendelea vyema baada ya marufuku ya FIFA kuondolewa.

Tangu mwaka 2022, ligi ya kandanda wanaume na wanawake imekuwa ikishabikiwa kwa ufanisi mkubwa kote nchini.

Hata hivyo, timu kadhaa zimekuwa zikikosa kushiriki mechi zao kutokana na ukosefu wa kifedha.

Klabu ya Mathare ambayo ilikuwa bingwa wa ligi kuu ya KPL mwaka wa 2008, ilishindwa kushiriki mechi tatu mfululizo mwaka 2022. Ilikosa kucheza mechi dhidi ya Bandari, Ulinzi Stars na Sofapaka hali iliyopelekea kushushwa kushiriki mechi za daraja ya chini.

Timu hiyo bado inaendelea kudidimia ikizingatiwa kuwa matokeo hayavutii. Kwa sasa ndio wanavuta mkia kwenye msimamo wa timu 18 za ligi ya kitaifa.

Timu nyingine ambayo imekabiliwa na matatizo kama haya hivi karibuni ni Vihiga Bullets ambayo ndio ya pili kutoka nyuma kwenye jedwali.

Uongozi wa klabu hii umeelezea wazi kulemewa kwake kifedha na tayari umetoa wito kwa wahisani kujitokeza kuwasaidia kuendesha shughuli zake.

Mnamo Jumatano, klabu hiyo ililemewa kusafiri kutoka nyumbani hadi Nairobi kucheza na AFC Leopards uwanjani Nyayo, Nairobi lakini kwa kutegemea hisani ya wasamaria wema waliweza kufanikiwa hatimaye.

Baada ya mechi hiyo ambapo walishindwa kwa bao moja pekee na wapinzani, vijana hao walikwama tena hadi pale Meya wa zamani wa Nairobi George Aladwa ambaye pia aliwahi kuwa naibu mwenyekiti na Katibu Mkuu wa klabu ya AFC Leopards, aliwanusuru na kuahidi kutumia umaarufu wake kuwatafuta marafiki wa kuinua timu hiyo hata baadaye.

Kando na klabu hizi mbili, kuna timu zingine ambazo zinapitia matatizo kama haya hata ingawa hazijafikia kiwango hiki cha kukosa chakula, nauli ya kufika viwanjani.

Ama kwa hakika, imeripotiwa mara nyingi jinsi ambavyo wachezaji wameendelea kukosa mishahara na marupurupu yao wakiwepo makocha wao. Gor Mahia na AFC Leopards ni mfano bora.

Wakati umefika sasa kwa waziri wa Michezo Ababu Namwamba kuingilia kati suala hili la ufadhili ili kuhakikisha klabu zinazoshiriki ligi za FKF zinapata mgao wa kifedha ambao unafaa na kwa wakati unaofaa.

Vivyo hivyo, viongozi na wafanyabiashara wafaa kujitolea kusaidia klabu hizi kiuchumi wakijua kuwa wema huu ni kwa manufaa ya vijana wetu.

Wanasiasa wafaa kumwiga gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ambaye majuzi alijitolea kufadhili klabu ya wanawake ya Falcons. Kiongozi huyo aliwapa chakula, malazi na makazi ya kufanyia mazoezi. Huu ndio mwelekeo bomba iwapo tunataka kufanikisha malengo ya soka nchini.

  • Tags

You can share this post!

Papa sasa atua Sudan Kusini kutafuta amani

DOUGLAS MUTUA: Vijana wafundishwe vya bwerere havitoshi kitu

T L