• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
TAHARIRI: Nani anafadhili majangili ambao wanaua maafisa wetu wa usalama?

TAHARIRI: Nani anafadhili majangili ambao wanaua maafisa wetu wa usalama?

NA MHARIRI

SIKU chache baada ya Taifa Leo kuandika taarifa iliyoonyesha kuwa wahalifu wanaikejeli serikali, majangili walishambulia maafisa wa polisi eneo la Kainuk kwenye barabara ya Lodwar-Kitale Jumamosi.

Kwenye shambulio hilo, majangili hao walifyatua risasi kutoka msituni kabla ya kuwavua nguo maafisa wa vikosi vya GSU, cha kupambana na wizi wa mifugo (ASTU) na wale wa RDU.

Baadaye walichoma mojawapo ya magari yaliyokuwa yamebeba maafisa hao. Wakati huo huo, majangili wengine walivamia kambi ya polisi katika Kaunti ya Laikipia.

Mashambulio haya yanayoendelezwa eneo la Rift Valley hayafai kuchukuliwa kuwa ni uhasama unaotokana na kuzozania rasilmali.

Wameonyesha kuwa hawaogopi mtu yeyote. Onyo la mara kwa mara kutoka kwa serikali kupitia Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki limekuwa kama kelele za chura. Majangili hao wanaonyesha kuwa wasiojali nchi, kwa kuvamia shule na kuzichoma na kufyatulia risasi magari barabarani. Sasa hivi wamefikia hatua ya kuwashambuliua maafisa wetu wa usalama na kuwavua nguo kwanza kabla ya kuwamiminia risasi.

Serikali inapaswa kuweka juhudi za haraka kukabiliana na majangili hao. Ikiwezekana, wakamatwe na kuwafichua watu wanaowadhamini. Haiwezekani kwamba majangili wanatawala maeneo ya Kaskazini mwa Rift Valley na kuua polisi, ilhali serikali ndiyo yenye uwezo wa kulinda wananchi.

Makundi yanayohangaisha raia katika baadhi ya nchi huanza kama magenge ya wahalifu wa kawaida kabla ya kubadilika kuwa majeshi ya waasi ambayo yangeshughulikiwa mapema na kuepuka hasara wanayosababisha.

Vitendo hivi mbali na kuonyesha kudharau mamlaka, ni ishara ya kuwa huenda jeuri waliyo nayo majangili ina msukumo kutoka pahali fulani.

Jana Jumapili akiwa mjini Nakuru, Rais William Ruto alikemea mashambulio hayo. Alimtaka waziri Prof Kindiki aendelee kupiga kambi katika maeneo husika hadi majangili hao wasambaratishwe.

Mbali na kutaka watu hao waangamizwe, itakuwa vyema pia kama serikali itawasaka na kuwakamata wanaofadhili uvamizi huu.

Bila hivyo, suala hili litakuwa janga lisilokuwa na mwisho. Ujasiri wa majangili hao unaonyesha kuwa hawa ni watu waliopata mafunzo ya hali ya juu.

Haiwezekani kwa jangili wa kawaida kuwa na uwezo wa kukabiliana na mchanganyiko wa vikosi vya usalama kwa zaidi ya saa nzima. Hawa lazima wawe watu waliopata mafunzo kuhusu vita.

Pia, ujeuri wao ni kama unachangiwa na kuwa wana mtu mwenye mamklaka anayewalinda. Kama si hivyo, inakuwaje watu hao wamekuwa wakiikejeli serikali kwa kushambulia punde tu waziri anapoondoka maeneo hayo?

  • Tags

You can share this post!

Chuo cha MKU-Rwanda chazindua kitabu kinachochora picha...

WANDERI KAMAU: Ungependa kukumbukwa vipi utakapoondoka...

T L