• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
TAHARIRI: Nguzo kuu ya dini ni utu bali si maisha ya baada ya kifo

TAHARIRI: Nguzo kuu ya dini ni utu bali si maisha ya baada ya kifo

NA MHARIRI

KWA sasa Kenya inaendelea kushtushwa na matukio ya vifo yanayoripotiwa katika dhehebu la Good News International, kijijini Shakahola, Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Idadi ya miili iliyofukuliwa inaelekea 100 huku ikiaminika vifo vinavyohusishwa na imani ya dhehebu hilo tata huenda vikawa mamia ya watu. Yapo makaburi mengi sana katika shamba la takribani ekari 800 la mhubiri wa dhehebu hilo, Paul Mackenzie Nthenge.

Hii ina maana kuwa shughuli ya kufukua miili ya wanaoshukiwa kufa baada ya kufunga kula na kunywa kwa siku nyingi, iliyoingia siku ya tano jana, huenda ikachukua muda mrefu zaidi.

Vifo hivi vimeibua maswali na haja ya kurejelea jukumu kuu na la kimsingi la dini au imani. Ijapokuwa dini nyingi hutofautiana kuhusu kinachofanyika kwa mwanadamu baada ya kufa, takribani zote zinakubaliana kuwa jambo la kimsingi kabisa liwe ubinadamu au utu ama wema wa muumini kwa binadamu mwenzake, wanyama na viumbe vingine vyote.

Dini zote halali zikiwemo zile za kiasili za Afrika, zinasisitiza matendo mema. Ukristo kwa mfano unasema, mtendee mwenzako jinsi wewe unavyopenda utendewe. Yaani usimdhulumu mwenzako wala kumtesa kwa sababu yoyote ile. Uislamu pia unahimiza wema na undugu. Bila kusahau dini za Kihindu na Kibudha zote zinatilia maanani matendo mema.

Hata hivyo, pameripotiwa matukio mbalimbali duniani kote na katika karibu dini zote kuwa yapo makundi katika dini hizi yenye itikadi kali. Katika Ukristo kundi la majuzi zaidi ni hili la mhubiri Mackenzie na katika Uislamu pameripotiwa makundi mbalimbali yenye misimamo mikali ya kidini kama vile Al Shabaab, Al Qaeda, ISIS na Boko Haram. Makundi haya yamebainika kuwafunza waumini wake kutenda matendo yanayosababisha vifo yakiwahadaa wanachama wayo kuwa ipo zawadi ahera.

Baadhi ya makundi hayo yanawadanganya waumini wa dini hizo kuwa ukiangamiza waovu kwa mlipuko wa kujitoa mhanga utatuzwa mabikira 72. Good News International nao wanasema ukifunga hadi kufa unaenda kukutana na Yesu Kristo moja kwa moja. Huo ni upotoshi mkubwa maadamu hao wanaowahubiria imani hizo wafuasi wao, nao wenyewe bado hawajafa kwa hivyo hawajui kwa hakika ni kitu gani hasa kinachowasubiri.

Hoja hiyo inaturejesha palepale mwanzoni; nguzo kuu ya dini ni nini? Ni matukio ya baada ya kifo au matendo mazuri duniani? Bila shaka jibu linakuwa matendo mazuri duniani. Yanayofanyika baada ya kifo yaachiwe Mungu.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali, maafisa wa polisi wasivuruge...

Raila kukaribishwa kwa heshima na taadhima atakaporejea...

T L