NA MHARIRI
NI jambo la fedheha kuwa Ukraine, nchi iliyozama katika vita vikali kwa mwaka mmoja uliopita, ni miongoni mwa nchi zinazoipa Kenya msaada wa chakula.
Nchi hiyo ya bara Uropa iliyo maarufu katika kilimo, imepanga kuipa Kenya tani 25,000 za ngano, ili hasa kusaidia katika mpango wa serikali wa kupunguza gharama ya chakula mbali na kuwaauni Wakenya walioathirika vibaya na njaa na ukame.
Katika mwaka mmoja uliopita, nchi hiyo haijashuhudia amani baada ya kuvamiwa na Urusi kwa mizinga, roketi na mabomu yasiyokoma. Hali hiyo imewakosesha raia wa taifa hilo utulivu kiasi kwamba hawawezi kuendelea na shughuli zao za kilimo jinsi inavyofaa.
Hii ina maana kuwa uzalishaji wa chakula nchini humo umepungua pakubwa.
Naam, wapo wanaoweza kusema kuwa labda Ukraine ina nia fiche inapotoa msaada huo. Inaweza kudhaniwa kuwa nchi hiyo ingependa Kenya iiunge mkono kuhusiana na janga la vita linalovuma nchini humo.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba taifa hilo lenye ukubwa unaokaribiana sana na wa Kenya, linalisha mataifa mengi duniani kutokana na kilimo chake. Ukraine ina ukubwa wa kilomita mraba 603,700 huku Kenya ikiwa na ukubwa wa 580,000. Tofauti ni kilomita mraba 23,000 pekee.
Mbona tutegemee chakula kinachotoka katika taifa linalotoshana na letu kwa ukubwa?
Upo uzembe wa viongozi wa Kenya katika masaibu yanayotatiza nchi hii na yakini mataifa mengine mengi ya bara Afrika.
Lazima tuzinduke! Ingawa ni kweli kwamba eneo kubwa la Kenya huwa jangwa au lenye ukame mkubwa (ASAL), sharti tuanze kufikiria jinsi taifa dogo sana la jangwani kama vile Israeli linavyojitegemea kwa chakula chake.
Miongoni mwa siri za ufanisi wa kilimo ni kuhakikisha yapo maji ya kutosha hata wakati ambapo mvua haipo. Hii ina maana sharti Kenya ianze kuhifadhi maji ya mvua na ikiwezekana kuelekeza baadhi ya maji ya maziwa katika maeneo kame. Ujenzi wa mabwawa makubwa ndio dawa mujarabu ya tatizo la njaa nchini.
Jambo la pili ni kuwahimiza wananchi wengi wajitose katika kilimo. Hili litawezekana vipi? Wakulima wapewe pembejeo zote kwa bei ya chini zaidi ili wanapovuna mazao yao, nao waweze kuyauza kwa faida. Miongoni mwa pembejeo hizo ni mbolea na mbegu.
Itakuwa muhimu, aidha kwa serikali ya Kenya Kwanza kuanzisha huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wakulima; wawe wakuzaji wa mazao au wafugaji wa wanyama. Mpango wa ushuri uliokuwa ukiendeshwa na maafisa wa nyanjani maarufu kama Extension Officers utawapa wakulima ushauri kuhusu magonjwa, mbegu, udongo na aina ya mimea ya kupanda katika maeneo yao.
Kwa kufanya hivyo, tutajiondoa katika fedheha ya kutegemea chakula kutoka nje.