• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
TAHARIRI: Raila asahau yaliyopita, Ruto asitumie mabavu naye

TAHARIRI: Raila asahau yaliyopita, Ruto asitumie mabavu naye

NA MHARIRI

KWA muda sasa, kinara wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga amekuwa akitishia kuisukuma serikali ya Rais William Ruto kutekeleza matakwa fulani.

Kati ya matakwa hayo ni kufungua sava za uchaguzi mkuu uliopita kwa lengo la kubaini mshindi halali wa kura za urais. Pia Bw Raila anataka Serikali ya Kenya Kwanza ipunguze gharama ya maisha inayotatiza Wakenya wengi.

Japo mengi ya matakwa hayo ni mazuri maadamu yanalenga kuwapunguzia raia mzigo wa maisha, takwa la kufungua sava huenda lisifaulu kwa sababu maji yakimwagika hayazoleki.

Ni sawa na tamathali “paka akiwa hakimu panya hawezi kushinda kesi”.

Katika muktadha huu, ‘paka’ ni Rais Ruto na ‘panya’ ni Bw Odinga. Kwa sababu hii, Bw Raila anafaa kufahamu kuwa hata kama ni kweli alishinda uchaguzi huo wa Agosti 9, hawezi kumpokonya Rais Ruto mamlaka.

Kwanza, iwapo ukweli ni huo, Dkt Ruto hawezi kukubali sava hizo zifunguliwe abadan katan.

Pili yamkini madai ya Bw Raila kuwa alishinda uchaguzi huo si kweli. Hali hizo mbili zinapowekwa kwenye mizani, inakuwa bayana kuwa Rais Ruto hawezi kukubali sharti hilo.

Kwa hivyo, Bw Raila anafaa kusahau takwa lake hilo maana yaliyopita si ndwele.

Hata hivyo, ni muhimu serikali ya Rais Ruto kutafuta kwa haraka njia ya kuwarahisishia Wakenya maisha. Gharama ya maisha imewalemea wengi, wengine wanachungulia kaburi.

Gharama ya umeme imepanda maradufu, ruzuku zote zilizowakinga raia wasiojiweza hasa kwa chakula zimeondolewa, nao ushuru umeongezeka zaidi. Karo ya shule iko juu.

Ukweli uliopo ni kwamba kufikia wakati ambao Kiongozi wa Taifa ameomba apewe ili aweze kutimiza baadhi ya ahadi zake za kurahisisha maisha ya Wakenya, wengi watakuwa wameangamia au wameporomoka kiasi cha kutoweza kujinyanyua maishani.

Hii ina maana kuwa takwa la Bw Raila kwamba serikali ipunguze gharama ya maisha upesi lina mashiko na linaungwa mkono na Wakenya wengi. Kwa hivyo, serikali haifai kuanza kutishia hatua za upinzani chini ya Bw Odinga za kulalamikia gharama ya maisha.

Mnamo Jumatano, serikali ya Kenya Kwanza iliweka vizuizi kwa kutumia magari ya polisi katika baadhi ya taasisi kuu za serikali, hasa jijini Nairobi na Kisumu. Vizuizi hivyo vilinuia kutibua mikakati ya upinzani dhidi ya Serikali.

Hilo halifai, maadamu hatua hizo za upinzani huenda si za kuzua vurugu.

Urekebishaji wa hali hii ya maisha unawezekana, tena kwa haraka. Iliwezekana mnamo 2003 pindi marehemu Mwai Kibaki aliposhika hatamu za urais. Inawezekana hata sasa.

  • Tags

You can share this post!

KIKOLEZO: TikTok inatesa, ndio, lakini Kenya haileti doo!

Kenya Power yajutia kitendo chake cha kukata umeme...

T L