NA MHARIRI
KATIKA mikutano yao tangu waingie Ikulu, Rais Ruto na naibu wake Gachagua wamekosa kutilia manani changamoto zinazokabili serikali yao, kiasi cha kushindwa kupunguzia raia mzigo mzito wa maisha.
Badala yake wameishi kulaumu MaBw Odinga na Kenyatta kwa masaibu ya raia.
Wamefeli kujenga mazingira tulivu yenye upendo, umoja na undugu bila moyo wa kisasi katika utawala wao mpya.
Wakenya walimaliza kazi debeni kwa kuwachagua wao na kukataa handisheki.
Mahasla walijidai jinsi watateuliwa mawaziri,makatibu na kushikilia nyadhifa za juu hasla mwenzao akiunda serikali.
Je, leo kuna mahasla wangapi katika Baraza la Mawaziri?
Muhimu wa Wakenya hata si vyeo serikalini bali matatizo yao kutatuliwa na matarajio yao kutimizwa kwa maisha ya bei nafuu. Mzigo wanaobebeshwa kwa sasa unaendelea kuwa mzito kama kito kila uchao.
Ikiwa hali ngumu itaendelea basi watajikuta wakifuata raia ya Bw Odinga kushiriki maandamano kulalamikia gharama ya juu ya maisha, bila kujali ikiwa walipigia kura utawala wa Kenya Kwanza au upinzani Azimio.
Serikali ijue Bw Odinga na viongozi wenzake wa upinzani wanatekeleza wajibu wao ipasavyo kuikosoa na kuisukuma.
Juhudi zao zinasaidia raia kujua haki zao na kuwapa ujasiri wa kukataa kutumiwa vibaya na serikali waliyochagua, hasa inaposhindwa kuwakwamua kutoka lindi la umaskini.
Rais Dkt William Ruto, naibu wake Bw Gachagua na wabunge wa Kenya Kwanza wakome kuzozana na Bw Odinga kwani ni utawala wao umefeli kutimiza ahadi ya kuteremesha bei ya bidhaa muhimu.